BAADA ya kusitisha mikataba ya makocha kutoka nchini Hispania, uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, uliziba pengo kwa kumwajiri Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, Januari 10 mwaka huu.

Mromania huyo tayari ametimiza wiki saba sasa tokea aanze kibarua chake akishirikiana na wasaidizi wake, Idd Nassor Cheche na Idd Abubakar, walioiongoza timu hiyo kutwaa taji la Kombe la Mapinduzi mwezi uliopita.

Kikosi cha Azam FC hivi sasa kipo kwenye kasi ya aina yake tokea mwaka huu uanze imecheza jumla ya mechi 14, ikiwa na rekodi ya kuruhusu wavu wake kuguswa mara moja tu, huku ikitwaa taji la Kombe la Mapinduzi kwa rekodi ya aina yake ya bila kufungwa mchezo wala kuruhusu wavu wake kuguswa.

Katika mechi hizo 14 ilizocheza mwaka huu, tano pekee ndizo za ligi ikiwa imeshinda tatu na kutoka suluhu mbili, tano za Kombe la Mapinduzi ikiwa imeshinda nne na suluhu mmoja, miwili mingine ya kirafiki ikiibuka kidedea mmoja kwa kuifunga Red Arrows (1-0) na suluhu dhidi ya Mabingwa wa Afrika Mamelodi Sundowns.

Ikiwa na safu kali ya ulinzi chini ya mabeki wa kati Yakubu Mohammed, Aggrey Morris na kipa Aishi Manula, ambao wamecheza asilimia 99.9 ya mechi za mwaka huu, imeshuhudiwa wakiruhusu bao moja tu walipoichapa Cosmopolitan mabao 3-1 kwenye mchezo wa Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup).

Mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz umefanya mahojiano maalumu na Cioaba ili kupata mambo mbalimbali na namna alivyojipanga kwenye kibarua chake hicho cha kuinoa Azam FC.

Uboreshaji kwenye timu na matokeo bora

Timu ya Azam FC imekuwa ikionyesha soka safi pamoja na kupata matokeo bora uwanjani hivi sasa, akizungumzia hilo Cioaba amesema kuwa hali hiyo inatokana na wachezaji kuelewa mbinu zake na mazoezi ya nguvu wanayofanya kila siku mazoezini.

“Sio kazi rahisi kwangu kwa wiki saba nilizokuwa hapa, ni muda mchache kwa kocha yoyote na si muda mrefu, katika kila mechi mimi na benchi langu la ufundi tumejitahidi kufanya kazi nzuri na kupata matokeo, wamekuwa msaada sana kwangu kuwajua wachezaji, nafasi na kila kitu kwa haraka sana.

“Kila mechi Azam FC imekuwa ikibadilika hatua kwa hatua, inacheza vizuri na kupata matokeo mazuri, lakini hilo haliwezi kuishia hapo nataka mbinu zangu, mipango yangu, niweze kuiweka zaidi kwenye hii timu na hapo baadaye Azam FC icheze soka la hali ya juu hapa Tanzania na kupata matokeo mazuri na hilo ndilo nalitaka zaidi,” alisema.

Anawazungumziaje wachezaji wa hapa

Akiwa amewahi kufundisha soka kwenye timu za baadhi ya mataifa kama vile Romania, Jordan, Kuwait, Oman, Saudi Arabia, Misri, Morocco na Ghana, Mromania huyo amedai kuwa Azam FC na Tanzania kwa ujumla ina wachezaji wengi wazuri huku pia akiisifu kiwango cha Ligi Kuu ya hapa.

“Si Azam FC tu ambayo nimeona wachezaji wazuri, nimewaona wengine kwenye timu zingine pia, soka la hapa liko vizuri hata ligi inaonekana kuwa nzuri, japo shirikisho la hapa (TFF) linatakiwa kuhakikisha timu zote zinakuwa na uwiano sawa wa mechi za nyumbani na ugenini, haiwezekani Simba na Yanga zisiende kucheza katika baadhi ya viwanja na kucheza mechi nyingi Uwanja wa Taifa, hii sio haki,” alisema.

Aina ya soka analopendelea

Cioaba ameshawahi kukaririwa na mtandao huu akieleza kuwa moja ya silaha zake kubwa ni soka la kushambulia na sio aina ya kocha anayependa timu yake icheze soka la kujilinda, safari hii amefafanua kiundani kuhusiana na namna anavyopenda timu yake iwe ikiwemo mfumo.

“Napenda soka la nguvu, kasi, napenda timu yangu kwenda sana eneo la kushambulia, mpira hivi sasa ni mchezo wa mbinu, kila timu inapenda kupata matokeo mapema, kama hauna mbinu nzuri uwanjani huwezi kushinda mchezo.

“Wakati mwingine mbinu zangu hutegemea na aina ya mpinzani ninayecheza naye, mara nyingine natumia 4-4-2, mara nyingine 4-2-3-1 na mara nyingine nacheza 4-3-3, na mfumo ambao napendelea ni 4-3-3, lakini kwa wakati huu ni ngumu kwa kuwa ni aina ya mfumo unaohitaji mazoezi mengi, mechi nyingi za kirafiki, na kwa sasa sina muda mrefu wa kubadilisha kwa sababu nimekuja ndani ya kipindi cha muda mfupi na timu ipo mashindanoni na kila wiki timu inatakiwa kucheza mechi,” alisema.

Anavyowapongeza wachezaji

Baada ya wachezaji wake kushika mafunzo yake haraka, Cioaba amechukua fursa hiyo kuwapongeza huku akidai kuwa wamekuwa wakifanya mazoezi kwa nguvu mazoezini jambo ambalo limeinua viwango vya wachezaji.

“Napenda kuwapongeza wachezaji, wamekuwa wakicheza kasi kama ninavyotaka, wamekuwa wakija mazoezini na mazoezi yamekuwa ni ya nguvu na kila mchezaji amekuwa akifanya kwa nguvu, hivi sasa kila mchezaji kiwango chake kimekuwa kikipanda, hili ni jambo zuri kwa timu.

“Kuna baadhi ya nafasi nina wachezaji wawili hadi watatu wote wakiwa wazuri, baadhi wamekuwa wakicheza na wengine kukaa benchi, kwa wachezaji ambao wamekuwa hawapo kwenye orodha, nimekuwa nikiwaambia nitampa kila mtu nafasi ya kucheza, lakini wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili siku nikiwapa nafasi wawe tayari,” alisema.

Cioaba alimtolea mfano winga Ramadhan Singano ‘Messi’, aliyempa nafasi kwenye nne zilizopita akisema kuwa kiwango chake kimekuwa kikiimarika jambo ambalo linazidi kumpa matumaini juu ya mwelekeo mzuri wa kikosi chake.

“Umemuona Messi kwenye mechi nne zilizopita nilizompa nafasi amekuwa akizidi kwenda juu na amefushafunga bao moja, kwenye kiungo vilevile Domayo (Frank) naye amekuwa akijaribu kufunga.

“Nina tatizo dogo kwenye ushambuliaji ambalo limeanza kulifanyia kazi nitawapa maelekezo ya jinsi gani ya kulekebisha tatizo hilo, umeona Bocco (John) alikuwa na bahati mbaya wiki nne ziliopita baada ya kuumia na sasa ndio amerejea, kila mmoja akielewa kila kinachoelekeza naamini mabao zaidi hapo baadaye” alisema.

Mipango michuano mitatu inayoikabili

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, ambaye ni baba mwenye mke na watoto wawili, alisema kuwa moja ya malengo yake makubwa ni kuifanya Azam FC kushinda katika kila mchezo wanyocheza katika michuano yote mitatu wanayoshiriki (Ligi Kuu, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika).

“Azam FC ina michuano mitatu muhimu sana, wa kwanza ni mtihani wa kwenye ligi, Azam FC hainafuraha kuwepo namba tatu katika msimamo, hii sio nafasi ya Azam FC, wachezaji wanatakiwa kutambua hilo na kila mtu anayeipenda Azam FC, kwa sasa tunapambana katika kila mchezo tunaocheza ili kukusanya pointi zote ili kukaa kwenye nafasi nzuri zaidi.

“Kuhusu Kombe la Shirikisho Afrika, hapa Tanzania zinacheza timu mbili kwenye michuano ya Kimataifa Azam FC na Yanga, mimi malengo yangu ni kwenda juu zaidi kwenye michuano hii, wiki ijayo nitakuwa na mchezo wa kwanza muhimu (Mbabane Swallows), wakati tukiwa kwenye maandalizi nitajaribu kuongea na kila mmoja kuwa makini kwenye mazoezi na katika mchezo ujao na naamini tutakuwa na matokeo mazuri katika michuano hiyo,” alisema.

Cioaba alidokeza kuwa tayari amepata taarifa mbalimbali kuhusiana na wapinzani wao Mbabane Swallows, ambao atacheza nao wiki ijayo kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Machi 12 mwaka huu kabla ya kurudiana nchini Swaziland Machi 19.

“Pia kuna michuano ya Kombe la FA (ASFC), ni moja ya michuano ambayo ipo kwenye mipango ya klabu, makocha, viongozi na kila mmoja, lengo ni kufika nusu fainali na hatimaye fainali na kubeba taji, naomba watu watambue kuwa mimi si aina kocha ninayependa kushika nafasi nne, ya tatu au ya pili,  napenda kuwa bingwa na nimejaribu kuwaambia wachezaji wajaribu kuwa makini katika kila mechi tunayocheza tuweze kuibuka na ushindi,” alisema.

Ijumaa iliyopita Azam FC iliweza kukata tiketi ya kuingia kwenye hatua ya robo fainali ya FA Cup baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, lililofungwa kiufundi na winga machachari anayerejea kwa kasi kubwa, Ramadhan Singano ‘Messi’.

Awatupia neno mashabiki

Cioaba ambaye amefurahishwa na namna mashabiki wanavyozidi kuongezeka kuja kuisapoti Azam FC, amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa anachoomba kutoka kwao ni kujitokeza kwa wingi zaidi uwanjani ili kuwaongezea morali wachezaji kuelekea mechi muhimu zinazokuja kuanzia mwezi huu.

“Huu ni mpira, kama unao mashabiki na wachezaji wakaona namna wanavyojitokeza kwenye mechi kuwasapoti inawakuwa inawapa nguvu zaidi uwanjani kwenye kupambana, kwa hapo baadaye katika mechi tatu hadi nne zijazo ni mechi muhimu sana kwa timu, inatakiwa wote tukae kwa pamoja, kuanzia uongozi, wachezaji, wafanyakazi na mashabiki, kama tutafanikiwa kwenye hilo naamini matokeo bora yatakuja,” alisema.

Azam FC ilivyomshangaza

Kocha huyo aliyewahi kuingoza Saham FC kutwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza nchini Oman msimu wa 2011-2012 na kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu, amesema kuwa hakutarajia kukutana hapa nchini na aina ya uwekezaji alioukuta Azam FC.

“Nilipata mshangao mkubwa nilipokuja mara ya kwanza hapa, Azam FC mbali na kufanya uwekezaji mkubwa, imekuwa ikiwapa mambo mazuri wachezaji wake, na kila kitu kipo ndani ya Azam FC, inachotakiwa hapo baadaye timu hii ni kuwa na matokeo mazuri, hii timu inatakiwa siku moja iwe timu bora hapa Tanzania kila msimu ishike nafasi ya kwanza, kama watu wataelewa mambo ninayotaka naamini hilo litafanikiwa,” alisema.  

Mambo mazuri anayokumbuka

Mbali na kuwahi kuipa taji Saham FC ya Oman, jambo jingine kubwa analokumbuka Cioaba ni kuiongoza Aduana Stars kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita.

Cioaba alisema kuwa wakati anakabidhiwa kikosi hicho timu hiyo ilikuwa imecheza mechi tano na kupoteza zote ikiwa nafasi ya mwisho kwenye msimamo, lakini aliweza kupambana na kupata matokeo bora yaliyoifanya timu hiyo kumaliza nafasi pili ikiwa pungufu ya pointi mbili na kinara wa ligi Wa All Stars.