BAADA ya maandalizi ya siku kadhaa kujiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo kamili kuelekea mtanange huo.

Mchezo huo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utafanyika leo Ijumaa ndani ya Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 10.30 jioni.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya mwisho jana jioni, Cioaba alisema kuwa kikosi chake kinamorali kubwa kuelekea mchezo huo na anamshukuru Mungu wachezaji wake wamefanya vema mazoezi ya mwisho.  

“Mazoezi ya leo yalikuwa mazuri, morali ipo ndani ya timu kuhusu mechi iliyopita tuliyocheza hapa ya ligi tulishinda 2-0 (Mwadui), kila mtu alikuwa makini kwenye mazoezi leo, lakini mchezo wa FA unatofauti na wa ligi, mchezo wa FA unahitaji mno umakini ndani ya mechi bila kufanya makosa na wachezaji kuingia uwanjani kufuata maelekezo niliyowaambia.

“Nawaamini wachezaji wangu watakuwa na mchezo mzuri kesho (leo) na kupata matokeo mazuri, baadhi ya wapo tayari sina wachezaji wengine waliokuwa majeruhi, Bocco (John) pekee ndio atakuwa akirejea baada ya kuwa majeruhi kwa wiki mbili au tatu zilizopita, lakini wiki hii ameanza mazoezi na nadhani ninaweza kumweka orodha ya wachezaji watakaokuwa katika mchezo huo,” alisema.

Mpaka sasa ni kiungo Stephan Kingue tu ambaye bado hajaanza mazoezi, akisumbuliwa na tatizo la kuchanika misuli ya nyama za paja kama Bocco, lakini yeye lake likiwa kubwa zaidi kuliko nahodha huyo.

Akiwazungumzia wapinzani wake, Cioaba alisema ameiona Mtibwa Sugar kuwa ni moja ya timu nzuri hapa Tanzania, lakini amejipanga kukabiliana nao ipasavyo kama alivyofanya kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mwadui.

“Unatakiwa kuwaheshimu wapinzani wako, lakini ninacheza nyumbani napenda kuendelea na mchezo wangu wa kwenda mbele na kucheza vizuri ili kupata matokeo mazuri na hilo ndio jambo muhimu,” alisema

Kocha huyo raia wa Romania, aliyekuwa akiinoa Aduana Stars ya Ghana msimu uliopita, aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti vijana wao jambo ambalo litawaongezea nguvu wakiwa uwanjani.

“Niliona mchezo uliopita (Mwadui), mashabiki walikuja wengi na kuisapoti timu, napenda kuwaambia mashabiki waelewe kuwa, hivi sasa benchi la ufundi, uongozi, wachezaji na mashabiki wanatakiwa kuwa pamoja kama familia na kufanya kazi pamoja ili kuifanya timu kwenda juu na kuwa na matokeo mazuri,” alimalizia.

Wakati hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola na Benki bora ya NMB, imejidhatiti vilivyo kufika hatua ya fainali na kutwaa taji hilo ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Msimu uliopita kwenye hatua kama hii iliwatoa Panone ya mkoani Kilimanjaro kwa jumla ya mabao 2-1, mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Ushirika.