BENCHI la kitabibu la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limeweka wazi hali za maendeleo ya wachezaji wawili waliomajeruhi hivi sasa, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na kiungo Stephan Kingue.

Nyota hao wawili wa Azam FC wanasumbuliwa na majeraha ya kuchanika misuli ya nyama za paja, lakini wote tayari wameshaanza mazoezi mepesi.

Wakati Bocco akianza mazoezi mepesi jana jioni, Kingue tayari ameanza programu ya mazoezi madogo madogo ya ‘gym’ na ya kukimbia kiasi pamoja na kuruka koni tokea katikati ya wiki iliyopita.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Daktari Mkuu wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa licha ya Bocco kuanza mazoezi mepesi bado yupo chini ya uangalizi wake huku akidai kuwa huenda akarejea uwanjani baada ya wiki mbili kuanzia sasa.

Mbali na Bocco, pia mtaalamu huyo amegusia hali ya kiafya ya Kingue akisema kuwa kiungo huyo tatizo lake limeonekana kuwa kubwa tofauti na Bocco na kudai huenda akarejea uwanjani baada ya wiki nne kuanzia sasa.

“Unajua mwili wa binadamu ni tofauti na gari, gari likiharibika inachukua muda mfupi kuweza kurejea kwenye hali yake ya kawaida, lakini mwili wa binadamu unahitaji tiba ya uhakika na muda kuweza kurejea kwenye hali ya kawaida,” alisema.  

Kikosi cha Azam FC hivi sasa kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Ijumaa ijayo saa 10.30 jioni.