USIKU wa kuamkia jana ulikuwa mzuri kwa kiungo wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, baada ya kuifungia timu moja ya mabao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Sure Boy alifunga bao hilo dakika ya 24 kwa shuti la umbali wa takribani mita 25 lililomshinda kipa wa Mwadui, Shaaban Kado na kuipa uongozi timu hiyo huku bao la pili likiwa ni la kujifunga kwa beki Iddy Moby, kufuatia mpira uliotemwa na kipa huyo kumgonga na kujaa wavuni.

Hilo ni bao la kwanza kwa Sure Boy msimu huu, na mara ya mwisho kuipatia Azam FC bao ilikuwa ni Machi 12 mwaka jana, wakati timu hiyo ilipoichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 3-0 kwenye mchezo wa awali wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) uliofanyika Uwanja wa Bidvest, jijini Johannesburg, nchini humo, nalo akipiga shuti kali nje ya eneo la 18.

Jambo jingine linalofurahisha ni mabao yote hayo mawili aliyofunga kiungo huyo mwaka huu na mwaka jana, yametokana na mchango wa winga Ramadhan Singano ‘Messi’, juzi akipewa pasi na winga huyo na kwenye lile dhidi ya Bidvest Wits, kona iliyochongwa na Singano ndiyo iliyozaa bao hilo lililokuwa la ufunguzi kwa Azam FC kwenye mchezo huo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Sure Boy alisema kuwa bao hilo ni zawadi tosha kwa mke wake, Amina Ramadhan, huku akidai kuwa umoja na mazoezi mazuri yaliyopo kwenye timu hiyo hivi sasa ndio chanzo cha kufanya vizuri mwaka huu ikiwa haijapoteza mtanange hata mmoja.

“Nampenda sana mke wangu (Amina Ramadhan), hilo bao nililofunga ni zawadi yake, hata nilivyocheza wakati nashangilia nimefanya kwa ajili yake na hilo linadhihirisha ni jinsi gani nampenda, nimekosa mechi mbili zilizopita za ligi, namshukuru Mungu kwa kurejea tena na kufanya vizuri,” alisema.

Kiungo huyo pia aliwaomba mashabiki wa Azam FC kuendelea kuwapa sapoti kwenye mechi zao huku akiwaahidi timu hiyo kuendelea kufanya vizuri na kuwasahaulisha yaliyotokea katika mzunguko wa kwanza wa ligi.