SASA ni wazi kuwa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki itacheza dhidi ya Mbabane Swallows Swaziland katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) utakaofanyika mwezi ujao.

Azam FC inakutana na timu hiyo baada ya Waswaziland hao kuwatoa Orapa United ya Botswana kwa mikwaju ya penalty 3-2 katika mchezo wa marudiano wa raundi ya awali uliofanyika kwenye Uwanja wa Mbabane nchini Swaziland.

Mchezo huo ulilazimika kwenda hatua ya changamoto ya mikwaju ya penalti kufuatia dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 kutokana na kila timu kushinda ugenini, Mbabane ikishinda 1-0 nchini Botswana kabla ya jana jioni nao kupigwa 1-0.

Azam FC iliyojiwekea malengo ya kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo mwaka huu, itaanza kuivaa timu hiyo nyumbani (Azam Complex) Machi 12 mwaka huu kabla kumalizia ng’we ya pili ugenini kati ya Machi 17,18 na 19.

Mshindi wa jumla wa mchezo huo, atasonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano (play off) na kukutana na moja kati ya timu 16 zitakazokuwa zimetolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi za kwanza zikifanyika kati ya Aprili 7, 8 na 9 na zile za pili zikipigwa kati ya Aprili 14, 15 na 16.

Timu zote zitakazopenya hapo, moja kwa moja zitakuwa zimeingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo safari hii kwa mara ya kwanza zitapenya timu 16 badala ya nane za huko nyuma, zitakazogawanywa katika makundi manne.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cole kinachoburudisha mwili na kuchangamsha koo pamoja na Benki bora nchini ya NMB, tayari imeshajiandaa vilivyo kuelekea michuano hiyo ikiwa imeshacheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki mwezi huu.

Ilianza kwa kukipiga na Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kutoka nayo suluhu (0-0) kabla ya mwanzoni mwa wiki hii kuichapa Red Arrows ya Zambia bao 1-0 katika mchezo wa mwisho wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.