IKICHEZA soka la hali ya juu, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeibuka kidedea baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex usiku huu.

Huo ni mwendelezo wa matokeo mazuri kwa timu hiyo tokea mwaka huu uanze, ambapo hivi sasa imefikisha jumla ya pointi 41 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi 10 na kinara Simba yenye pointi 51 ambayo ina mchezo mmoja mkononi.

Tokea raundi ya pili ianze Azam FC imecheza jumla ya mechi nane, ikishinda nne na kutoka suluhu nne, ikiwa haijaruhusu wavu wake kuguswa kutokana na uimara uliopo kuanzia eneo la ukabaji katikati ya uwanja hadi eneo la ulinzi linalooongozwa mabeki wa kati, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed huku kwenye milingoti mitatu akiwa kipa Aishi Manula.

Mabao pekee ya Azam FC kwenye mchezo huo yalifungwa na kiungo Salum Abubakar na beki wa Mwadui, Iddy Moby, aliyejifunga wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira uliotemwa na kipa wa Mwadui, Shaaban Kado, aliyekuwa akiokoa krosi iliyochongwa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Kabla ya kuanza mchezo huo, timu zote mbili pamoja na mashabiki waliohudhuria walisimama kimya kwa dakika moja kama ishara ya kuomboleza kifo cha kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Tukuyu Stars, Tanzania Prisons na Yanga, Geoffrey Boniface Mwandanji, aliyefariki dunia katikati ya wiki hii, huku pia zikivaa vitambaa vyeusi begani.

Azam FC ilionyesha dalili njema mapema tu ya kusaka ushindi kwenye mchezo huo baada ya kutandaza soka la hali ya juu ikilishambulia kwa kasi lango la Mwadui kwa kugongeana pasi, lakini safu ya ulinzi ya timu ilisimama imara kuondoa hatari zote.

Azam FC ilikaribia kuandika bao la uongozi dakika ya 10 baada ya kufanya shambulizi kali langoni mwa Mwadui, lakini kichwa kilichopigwa na Yahaya Mohammed kufuatia krosi ya beki Shomari Kapombe, kilipanguliwa vema na kipa wa Mwadui na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi, waliendelea kulipa kashikashi lango la wapinzani wao na hatimaye dakika ya 24 shuti kali lililopigwa na Abubakar umbali wa mita 25 lilimshinda kipa wa Mwadui na kujaa wavuni.

Singano aliyeendeleza kiwango chake bora kwenye mechi ya pili mfululizo baada ya ile ya katikati ya wiki dhidi ya Red Arrows, aliipenya ngome ya ulinzi ya Mwadui dakika ya 36 lakini shuti alilopiga liliishia mikononi mwa kipa wa Mwadui.

Hadi zinamalizika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Azam FC ilitoka kifua mbele uwanjani ikiwa na uongozi wa bao hilo.

Kipindi cha pili ilianza tena kwa kasi yake na dakika ya 47 beki Yakubu Mohammed, alikaribia kufunga bao jingine baada ya kupiga kichwa kizuri kilichotoka sentimita chache ya lango kufuatia mpira mzuri wa faulo uliochongwa na Singano kufuatia kufanyiwa madhambi na mabeki wa Mwadui.

Azam FC ilijipatia bao lake la pili dakika ya 88, likiwa ni la kujifunga la beki wa Mwadui, Moby, kufuatia mpira uliopanguliwa na kipa wa timu hiyo kufuatia krosi ya Singano kumgonga na kujaa wavuni, bao ambalo liliihakikishia pointi zote mabingwa hao.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC inatarajia kuendelea na programu ya mazoezi kama kawaida kesho kujiandaa na mtanange wa raundi ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Ijumaa ijayo saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Himid Mao (C), Frank Domayo, Joseph Mahundi/Abdallah Masoud dk 70, Ramadhan Singano, Salum Abubakar/Samuel Afful 63, Yahaya Mohammed/Erasto Nyoni dk 88