KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumapili inatarajia kushuka tena dimbani kuvaana na Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wamekuwa wakifanya maandalizi makali kuelekea mchezo huo yote hayo ni kuhakikisha inazoa pointi zote tatu ili kuzidi kujiongezea pointi, ambapo mpaka sasa imejikusanyia 38 katika nafasi ya tatu nyuma ya pointi 13 dhidi ya kinara Simba aliyejikusanyia 51.

Timu hiyo inayodhaminiwa na kinywaji safi kinachochangamsha mwili ambacho ni burudani kwa koo lako cha Azam Cola pamoja na Benki inakimbiza hapa nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, iliichapa timu hiyo mabao 4-1 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika mkoani Shinyanga.

Mchezo huo wa kesho utakuwa ni wa nne kwa Azam FC kucheza na Mwadui katika ligi tokea timu hiyo ipande daraja, ambapo imeifunga mara zote timu hiyo ikiwa imetupia mabao sita na kuruhusu wavu wake kuguswa mara moja tu.

Mbali na mechi ya ligi, timu hizo zimewahi kukutana kwenye nusu fainali ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) na Azam FC ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia ndani ya dakika 120 za mchezo huo timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2, mabao yote ya mabingwa hao yakiwekwa kimiani kiufundi na Khamis Mcha ‘Vialli’.

Pia walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu uliopita uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, bao pekee la Azam FC likifungwa na Ramdhan Singano ‘Messi’ huku lile la Mwadui likifungwa na Bakari Kigodeko.

Kama ilivyokuwa katika mechi mbili zilizopita za ligi, Azam FC itaendelea kuwakosa wachezaji wawili nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na kiungo Stephan Kingue, ambao bado wanauguza majeraha yao ya misuli ya nyama za paja, lakini itakuwa na urejeo wa kiungo Salum Abubakar, aliyepona maumivu ya mguu yaliyokuwa yakimkabili.

Rekodi baab’kubwa Azam FC

Azam FC inaingia kwenye mchezo ikiwa na rekodi bora mpaka sasa tokea mwaka huu uanze ikiwa haijafungwa mchezo wowote katika mechi 12 ilizocheza, huku ikiwa imetwaa taji la Kombe la Mapinduzi kwa rekodi ya aina yake ya bila kufungwa mchezo wala kuruhusu wavu wake kuguswa.

Katika mechi hizo 12 ilizocheza mwaka huu na kuruhusu bao moja tu, nne pekee ndizo za ligi ikiwa imeshinda mbili na kutoka suluhu mbili, tano za Kombe la Mapinduzi ikiwa imeshinda nne na suluhu mmoja, miwili mingine ya kirafiki ikiibuka kideda mmoja kwa kuifunga Red Arrows (1-0) na kutoka suluhu mmoja dhidi ya Mabingwa wa Afrika Mamelodi Sundowns.

Mchezo pekee ambao imeruhusu bao ni ule wa Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) waliocheza dhidi ya Cosmopolitan na kuifunga mabao 3-1, ushindi ulioifanya kutinga hatua ya 16 bora watakayocheza na Mtibwa Sugar Ijumaa ijayo (Februari 24).

Ili kudhihirisha ubora waliokuwa nao mwaka huu, Azam FC imezifunga timu zote kongwe za Simba (1-0) na Yanga (4-0), ikizipiga katika Kombe la Mapinduzi na kutwaa taji hilo kabla ya kuipiga tena Simba kwenye ligi bao 1-0, lililofungwa na Bocco, aliyefikisha bao lake la 19 dhidi ya wekundu hao katika mechi mbalimbali.

Mara ya mwisho Azam FC kupoteza mechi ilikuwa Novemba 6 mwaka jana ilipofungwa bao 1-0 na Mbao katika mchezo wa ligi uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, lakini tokea hapo imekuwa na uwiano mzuri wa kupata matokea bora katika mechi zake mbalimbali.

Mechi za Azam FC 2017

Ligi Kuu (VPL)

Wed 18/01/17 Azam FC 0 – 0 Mbeya City       

Sat  28/01/17  Simba SC 0 – 1 Azam FC

Sun 05/02/17  Azam FC  1 – 0 Ndanda

Sat 11/02/17 Ruvu Sh/t   0 – 0 Azam FC

Kombe la Mapinduzi

Mon 02/01/17 Azam FC 1 – 0 Zimamoto

Wed 04/01/17 Jamhuri   0 – 0 Azam FC

Sat   07/01/17 Yanga     0 – 4 Azam FC

Tue 10/01/17 Azam FC 1 – 0 Taifa Jang’ombe (Semi)

Fri  13/01/17 Azam FC  1 – 0 Simba SC (Final)

FA Cup

Fri 24/01/17 Azam FC    3 – 1 Cosmopolitan

Mechi za kirafiki

Thur 02/01/17 Azam FC 0 – 0 Mamelodi Sundowns

Wed 15/02/17 Azam FC 1 – 0 Red Arrows