KOCHA Mkuu wa Mabingwa wa zamani wa Zambia Red Arrows, Honor Janza, ameitabiria makubwa Azam FC kufika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.

Kauli ya Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’, imekuja saa chache mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki baina ya timu hizo, uliomalizika kwa Azam FC kushinda bao 1-0.

“Azam FC kiufundi ipo vizuri wanaweza kwenda mbele, kwangu mimi nawatakia mafanikio mema, kwa sababu aina soka nililoliona wanacheza ni ngumu kuliona kwenye timu za Afrika, huwezi kuona timu nyingi zikicheza aina hii ya soka la hali ya juu, unaweza kuliona katika soka la Kimataifa,” alisema.

Janza alisema kuwa ana uzoefu wa kufundisha ngazi mbalimbali za soka barani Afrika kama vile timu ya Taifa ya Zambia kwenye fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2015 nchini Guinea ya Ikweta, hali ambayo inampa matumaini makubwa kwa kuipa nafasi timu hiyo kufika mbali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

“Azam FC kama ikiendelea kucheza aina ya soka hili inalocheza nafikiri timu hii itafika mbali sana, ina nafasi ya kufika robo fainali ya michuano hiyo hivi sasa nakubaliana kwa nini timu hii iliweza kuihodhi Mamelodi Sundowns (Mabingwa wa Afrika).

“Kwa sababu aina ya soka inalocheza Azam FC linafanana kwa kiasi kikubwa na lile ya Sundowns, wako na kasi, wanaenda mbele, wanauwezo wa kumiliki mpira, pia wana uwezo wa kuurudisha mpira kwa haraka na kuumiliki pale wanapoupoteza, na hivi ndivyo soka la kisasa lilivyo, kama unaweza kucheza soka la kasi, soka la akili, soka la kushambulia, kuzuia kama timu na hivi ndivyo soka lilivyo,” alisema.

Kocha huyo aliyetoka kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Taifa ya Zambia kabla kutua Red Arrows mwezi uliopita, aliipa ushauri Azam FC kama inataka kwenda mbele zaidi akisema kuwa lazima iendelee na mtiririko wa aina ya soka wanalocheza hivi sasa, falsafa yao, huku akiamini ya kuwa kwa namna hiyo watapata mafanikio mengi hapa Tanzania.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi, wanaodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola na Benki bora nchini ya NMB, wanatarajia kuanzia raundi ya kwanza ya michuano hiyo kwa kukipiga na moja ya timu kati Mbabane Swallows ya Swaziland na Orapa United ya Botswana kati ya Machi 10 na 12 nyumbani kabla ya kumalizia ngwe ya pili ugenini kati ya Machi 17 na 19.

Wamevuna nini Tanzania?

Wakati wakitarajiwa kuondoka nchini kesho Ijumaa usiku baada ya kukamilisha ziara yao leo, Janza ameweka wazi kuwa vijana wake wamejifunza mengi kupitia mchezo huo na wameahidi kuwa watachukua baadhi ya vitu kwa ajili kuvifanyia kazi kwenye ushindani wa soka wa Ligi Kuu ya Zambia.

“Nimeongea na vijana wangu kuwa aina ya soka linalihitaji ni kama hili lililoonyeshwa na Azam FC na wamekubali soka la aina hii la hali ya juu na kasi, pia unatakiwa kumiliki mchezo kama ulivyojionea Azam FC ilivyomiliki kwa muda mrefu na kwa malengo, huwezi ukamiliki mchezo tu bila malengo.

“Hivyo unaumiliki kwa malengo kwa kwenda mbele, kama kocha nawashukuru sana Azam FC wametupa mazoezi mazuri, kama kocha na wachezaji wangu tumejifunza mengi, hongera sana Azam FC na waendelee kuwa juu,” alimalizia.