BAO pekee la Azam FC lililowekwa kimiani na beki Abdallah Kheri, limetosha kabisa kuizima Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Wakati Azam FC ikiutumia mchezo huo kama maandalizi kuelekea mechi yake ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, Arrows iliyoweka kambi hapa nchini yenyewe imeutumia mtanange huo kama kipimo tosha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Zambia.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya bora kabisa nchini ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, itaanza kufungua dimba kwenye michuano hiyo kwa kuvaana na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali kati ya Mbabane Swallows ya Swaziland na Orapa United ya Botswana.

Kwa mara ya kwanza tokea asaini mkataba wa kuinoa Azam FC Januari mwaka huu, Kocha Mkuu Aristica Cioaba, aliweza kukaa benchini maara baada ya jana kupata rasmi kibali cha kufanya kazi nchini, akisaidiana na Kocha Msaidizi, Idd Nassor Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar.

Cioaba alitumia vikosi viwili tofauti kwenye mchezo huo na vyote vikionekana kucheza vema, hali ambayo iliwafurahisha mashabiki waliohudhuria kushuhudia mchezo huo ndani ya viunga vya Azam Complex.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi, waliofanikiwa kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo walionekana kwa vipindi vyote wakicheza soka la kasi, pasi pamoja na kukaba kwa haraka kila walipopoteza mpira.

Kutokana na kasi hiyo huenda wangejipatia bao la mapema dakika ya 13, kama Ramadhan Singano ‘Messi, angeiwahi na kuimalizia vema krosi safi aliyopigiwa na beki wa kulia Shomari Kapombe, aliyeambaa na mpira kwa kasi na kuwahadaa mabeki wa Arrows kabla ya kupiga krosi hiyo.

Dakika ya 34 Yahaya alijaribu kuwatoka wachezaji wanne wa Arrows na kuingia kwenye eneo la 18, lakini pasi aliyopiga ilishindwa kumaliziwa vema na Shaaban Idd, aliyepiga shuti liliokolewa na mabeki na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda na kushuhudiwa dakika 45 za kipindi cha kwanza kikimalizika kwa suluhu.

Kipindi cha pili Azam FC iliendelea na kasi iliyoanza kipindi cha kwanza, hasa winga wa kushoto Ramadhan Singano, aliyeonekana kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri kutokana na kasi yake na uwezo mkubwa wa kuitoka ngome ya timu pinzani na kupiga pasi za hatari.

Dakika ya 60, benchi la ufundi la Azam FC lilifanya mabadiliko ya kikosi kizima kwa kuwaingiza wachezaji wapya na kukipumzisha kikosi kilichoanza kwenye mchezo huo, mabadiliko ambayo yaliizidishia kasi timu hiyo hasa wachezaji Enock Atta Agyei, Abdallah Masoud, Salum Abubakar, Erasto Nyoni, Khamis Mcha, wakionekana kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.

Madhambi aliyofanyiwa Atta dakika ya 83 pembeni ya uwanja mita chache nje ya eneo la 18 kwenye usawa wa eneo la kibendera, ndiyo yaliyozaa bao la Azam FC dakika ya 84 baada ya Mcha kupiga mpira safi wa adhabu ndogo uliomaliziwa kwa kichwa na Kheri, ambaye katika mchezo huo alicheza kama kiungo mkabaji.

Azam FC ilipata pigo katika dakika nne za mwisho za nyongeza baada ya winga wake wa kushoto, Enock Atta, kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kisha moja kwa moja nyekundu kufuatia kile kilichodaiwa na mwamuzi wa mchezo huo, Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam, ya kuwa alikuwa akipoteza muda kwenye mpira wa kurusha kuelekea langoni mwa Arrows.

Arrows inayonolewa na Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia, Honor Janza, licha ya kufungwa mchezo huo, nayo ilionyesha upinzani mkali na soka zuri lakini ilishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza huku pia ikikutana na safu ngumu ya ulinzi ya Azam FC kwa vipindi vyote viwili.

Timu hiyo ya Jeshi la Anga la nchini Zambia, itamaliza ziara yake nchini leo Alhamisi kwa kufanya mazoezi ya mwisho ya ufukweni kabla ya kesho Ijumaa usiku kuondoka nchini kurejea Zambia kwa ajili ya maandalizi ya mwisho mwisho kuelekea msimu mpya wa ligi ya nchi hiyo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza rasmi mazoezi leo Alhamisi saa 1.00 usiku kujiandaa na mtanange ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex muda kama huo Jumapili ijayo.

Vikosi cha Azam FC leo hii:

Aishi Manula/Mwadini Ally dk 60, Shomari Kapombe/Erasto Nyoni dk 60, Bruce Kangwa/Gadiel Michael dk 60, Yakubu Mohammed/David Mwantika dk 60, Aggrey Morris/Ismail Gambo dk 60, Himid Mao (C)/Abdallah Kheri dk 60, Frank Domayo/Abdallah Masoud dk 60, Yahaya Mohammed/Samuel Afful dk 60, Shaaban Idd/Salum Abubakar dk 60, Joseph Mahundi/Khamis Mcha dk 60, Ramadhan Singano/Enock Atta dk 60