MABINGWA wa zamani wa Zambia, Red Arrows, walioweka kambi hapa nchini, wamewamwagia sifa wenyeji wao Azam FC kutokana na namna ilivyojipanga na miundombinu inayojitosheleza.

Arrows iliyotwaa taji la ligi hiyo mwaka 2004, imetua nchini tokea mwanzoni mwa wiki iliyopita kwa kambi maalumu ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zambia.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz wakati wa mazoezi ya timu hiyo, Kocha Mkuu wa Arrows, Honor Janza, alisema kuwa timu hiyo imejipanga vema kuanzia kwenye eneo la uongozi, programu na mazoezi.

“Sisi tuko hapa kwa ajili ya kujijenga, unajua Azam FC ni timu bora na yenye ujuzi, ni timu iliyoko kwenye michuano ya Afrika, tumeiona ni timu iliyojipanga, inaonekana ipo na ujuzi zaidi, wamejipanga kuanzia kwenye uongozi, programu za kila siku na mazoezi, sisi tunajisikia furaha kujihusisha na klabu kama hii na sisi tunataka kuingia kwenye njia kama yao,” alisema.

Kocha huyo alisema kuwa wanajisikia furaha sana kupewa nafasi na uongozi wa timu hiyo wa kutumia miundombinu ya Azam FC kwa siku zote wanazokaa hapa nchini, huku akisifia kuwa ni miundombinu ya hali ya juu.

“Tumefurahia sana miundombinu ya Azam FC tunayoendelea kutumia, kiukweli tunajisikia kama tupo nyumbani ni nzuri kwa klabu yetu na wachezaji wetu, tunapenda kumshukuru kocha wa timu hii, benchi la ufundi, wachezaji, wafanyakazi, Azam kama kampuni na uongozi kwa ujumla, wamekuwa msaada sana kwetu, tumekuwa tukipata kila kitu kwa wakati, Maji na huduma nyingine tunazohitaji,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’, alimalizia kwa kusema kuwa wanatarajia kuwapa mazoezi mazuri Azam FC katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika kesho Jumatano saa 1.00 usiku ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

“Azam FC itegemee mchezo mzuri kesho, tutawapa mazoezi mazuri sana kesho kwa ajili ya wao kufanya vizuri katika mechi za Afrika (Kombe la Shirikisho Afrika) na ligi, sisi hatutaangalia ushindi kwenye mchezo huo, tunataka kuchaji nguvu zetu, mbinu zetu, kuangalia aina ya soka letu, ustahimilivu kwenye mechi, Je, tunaweza kuhimili dakika 90 pamoja na mambo mengine ya kiufundi,” alisema.

Arrows tokea iwasili nchini imekuwa ikitumia miundombinu ya klabu ya Azam FC, kama vile uwanja, gym, bwawa la kuogelea, yote hayo ni katika kufanya maandalizi yao mazuri kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Zambia.