KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa kutokuwa vizuri kwa eneo lake kiungo na ushambuliaji ndiko kumepelekea matokeo ya suluhu dhidi ya Ruvu Shooting jana.

Suluhu hiyo kwenye mchezo wako huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Pwani umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 38 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nyuma ya pointi 13 dhidi ya vinara Simba waliojikusanyia 51.

Cheche ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo kuwa, mbali na tatizo hilo pia amedai kuwa ubovu wa Uwanja wa Mabatini, nao uliwanyima nafasi ya kucheza hasa ukiwanyima uhuru wachezaji wake.

“Kwanza tunamshukuru Mungu kwa kumaliza mchezo salama kwa kutopata maumivu wachezaji wangu, hilo ndio jambo kubwa lakini pili nasikitika kwa sisi kutopata ushindi kwenye mchezo huu, tatu safu yangu hasa kuanzia eneo la kiungo kwenda mbele haikuwa vizuri kwenye mchezo huu na kupelekea kushindwa kupata bao.

“Lakini hili huwa linatokea kwenye mechi, timu haiwezi kuwa vizuri kila siku hali hii tutaifanyia kazi ili isijirudie kwenye mechi ngingine, na mwisho uwanja nao vilevile umetunyima sehemu fulani ya fursa, lakini ni mambo ambayo yanaweza kutokea kwenye mchezo tumeyakubali na tutaenda kuyafanyia kazi,” alimalizia.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachochangamsha mwili na koo lako pamoja na Benki ya NMB, mara baada ya mchezo huo, wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja na watarejea mazoezini kesho Jumatatu asubuhi kujiandaa na mechi zijazo.

Itakumbukwa kuwa Jumatano ijayo, Azam FC itashuka dimbani kumenyana na Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuanzia saa 1.00 usiku.

Arrows ambayo ipo nchini chini ya wenyeji wao Azam FC, imeweka kambi maalumu ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zambia na imekuwa ikifanya mazoezi kila siku kwenye miundombinu ya Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC itautumia mchezo huo kama sehemu ya maadalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo inatarajia kufungua pazia mwezi ujao kwa kukipiga na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.