KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya bila kufungana na wenyeji wao, Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani jioni ya leo.

Sare hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 38 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo, ikizidiwa pointi 13 na vinara Simba waliofikisha pointi 51 baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 3-0.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu, nahodha John Bocco, viungo Salum Abubakar na Stephan Kingue, ambao wote ni majeruhi.

Lakini beki Bruce Kangwa, aliyekuwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Gabon na timu yake ya Taifa ya Zimbabwe, aliyerejea kikosini kwa mara ya kwanza tangua acheze mechi ya mwisho dhidi ya Majimaji Desemba mwaka jana.

Kwa kiasi kikubwa mchezo wa leo, uliathiriwa na uwanja mbovu wa Mabatini, hali iliyozifanya timu zote mbili kutumia mipira mirefu wakati wa kupanga mashambulizi na kupelekea utengenezaji wa nafasi kuwa finyu.

Uwanja wa Mabatini umeonekana kuwa na kasoro kadhaa katika eneo la kuchezea, mbali na nyasi zake kutokuwa katika hali nzuri pia umeonekana kutokuwa na usawa (baadhi ya sehemu zikionekana kuwa na miinuko midogo), hali ambayo imefanya eneo la kiungo kukosa ubunifu hasa pale wanapomiliki mpira.

Azam FC ilianza kutengeneza nafasi nzuri ya kwanza dakika ya 18, kwa mpira wa mzuri wa kona uliochongwa na nahodha wa mchezo wa leo, Himid Mao, lakini mshambuliaji Yahaya Mohammed alishindwa kutumia vema nafasi hiyo baada ya shuti alilopiga kupaa juu ya lango la Ruvu Shooting.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi walilazimika kufanya mabadiliko dakika ya 53 baada ya kiungo Frank Domayo kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na beki Shomari Kapombe, hali ambayo ilimlazimu Erasto Nyoni aliyekuwa akicheza beki ya kulia kuhamia eneo la kiungo kuziba mahali pa Chumvi.

Kipa Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada dakika ya 57 baada ya kuokoa mchomo mkali ya Jabir Aziz aliyepiga shuti hilo ndani ya eneo la 18 na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kucheza na Red Arrows

Mara baada ya kumalizika mchezo huo, Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Jumatano ijayo kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Red Arrows ya Zambia, iliyokuja nchini kuweka kambi maalumu ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zambia, utakaoanza saa 1.00 usiku ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC itautumia mchezo huo kama sehemu ya maadalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo inatarajia kufungua pazia mwezi ujao kwa kukipiga na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Arrows iliyowahi kufundishwa na Kocha wa Yanga, George Lwandamina kabla ya kutimkia Zesco United, ipo nchini chini ya wenyeji wao Azam FC, ambapo wamekuwa wakitumia miundombinu ya timu hiyo ndani ya makao makuu yake ya Azam Complex, kwa kufanyia mazoezi tokea iwasili nchini mwanzoni mwa wiki hii.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Himid Mao (C), Frank Domayo/Shomari Kapombe dk 53` , Joseph Mahundi/Masoud Abdallah dk 46, Bruce Kangwa, Samuel Afful/Shaaban Idd dk 77, Yahaya Mohammed