BEKI wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa hali yake ya kiafya ipo vizuri kuendelea kuwapigania mabingwa hao kuelekea mechi zijazo.

Kauli hiyo ya Kapombe imekuja siku chache mara baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa, beki huyo amerudiwa na ugonjwa wake wa msimu uliopita, wa donge la damu kuganda kwenye mishipa ya damu katika mapafu (Pulmonary Embolism).

Beki huyo wa Kimataifa wa Tanzania, alilazimika kupelekwa jijini Cape Town, Afrika Kusini katika Hospitali ya Vincent Pallotti, ili kufanyiwa matibabu ya kina na hatimaye hali yake kuimarika na kuanza kucheza msimu huu.

Kutokana na taarifa hizo, Kapombe amekuwa akipigiwa simu na ndugu zake mbalimbali pamoja na rafiki wakimjulia hali na kumuuliza kuhusiana na habari hizo, jambo ambalo amekuwa akilikanusha kwa kila anayempigia.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kapombe alisema kuwa alikosekana kwenye mechi mbili zilizopita kutokana na daktari wake aliyempatia matibabu awali kumtaka aende akamfanyie tena uchunguzi kujua maendeleo ya afya yake.

“Nilikosa mechi hizo kutokana na tarehe zangu za kwenda kufanyiwa uchunguzi nchini Afrika Kusini kuhusiana na ugonjwa wangu wa awali kufika, daktari aliyenitibu (Dr. Chapman) alikuwa ananihitaji, kwa hiyo nikaenda kufanya uchunguzi na majibu niliyopata ni mazuri, nimerudi afya yangu ipo vizuri, nilifanyiwa vipimo vingi vikiwemo vya damu na ule ugonjwa na mambo yote yalionekana yapo vizuri na afya yangu kwa ujumla ipo vizuri,” alisema.

Beki huyo alisema kuwa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna anavyozidi kumsimamia, huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo waliopata hofu awali juu ya afya yake baada ya kuona taarifa kwenye magazeti waamini ya kuwa yupo vizuri.

“Mashabiki walioniona sipo kwenye timu na nimekosa mechi mbili, wakajua labda naumwa, lakini siyo kama magazeti yalivyoandika, nilienda kufanyiwa uchunguzi na sasa nimerejea na nipo tayari kucheza mechi zilizobakia,” alisema. 

Kapombe ambaye yupo na kikosi cha Azam FC kinachojiandaa na mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, amesema kuwa yupo vizuri kwa ajili ya mchezo huo lakini uwepo wake uwanjani utategemeana na mahitaji ya kocha kuelekea mtanange huo.

“Naendelea kufanya mazoezi vizuri, nimefanya wiki yote hii vizuri na mpaka leo hii mwisho wa mazoezi haya nimefanya vizuri,” alisema

Daktari naye anena

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, naye alilitolea ufafanuzi suala hilo akisema kuwa hali ya Kapombe ipo vizuri baada ya kufanyiwa vipimo tena kuhusiana na maendeleo ya afya yake.

“Muda wote Kapombe alikuwa akitumia dawa za kuondoa donge hilo la damu au kusababisha donge hilo lisizidi kuwa kubwa zaidi, alikuwa akicheza mpira na kutumia hizo dawa, kwa hiyo wiki iliyopita tukaona ni muhimu yeye kwenda kufanyiwa uchunguzi, na kwa bahati nzuri alivyofanyiwa uchunguzi lile donge la damu kwenye mishipa ya damu sasa halionekani, kwa hiyo Kapombe hivi sasa amerejea mazoezini kwa asilimia 100 kwa hiyo hilo ndilo lilikuwa tatizo lake,” alisema.

Mwankemwa aliongeza kuwa: “Lakini sasa Kidaktari, hatukujua hasa lile donge linaweza kujirudia tena au la, hivyo bado daktari (Dr. Chapman) kule Afrika Kusini katika Hospitali ya Vincent Palloti, ameendelea kushauri kuwa aendelee kutumia vidonge vya kuzuia damu kuweza kuganda, kwa hiyo Shomari Kapombe anafanya mazoezi kama kawaida anacheza kama kawaida, lakini ataendelea kutumia hizo dawa.”

Alimalizia kwa kusema kuwa, Kapombe alikutwa na tatizo la nyonga na Daktari Nickolas wa hospitali hiyo, ambalo tayari amepatiwa matibabu yake.