BAADA ya kupenya kwenye raundi ya 16 ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepangiwa kucheza na Mtibwa Sugar katika kuwania robo fainali ya michuano hiyo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa leo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeonyesha kuwa mchezo huo utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Ijumaa ya Februari 24 mwaka huu.

Azam FC ilitinga hatua hiyo baada ya kuifumua Cosmopolitan mabao 3-1, yaliyofungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Joseph Mahundi na Shaaban Idd na kuizima kabisa timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL).

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wamejipanga vilivyo kufanya kweli kwa kutwaa taji kwenye michuano ya mwaka huu kufuatia msimu uliopita kushika nafasi ya pili baada ya kufungwa mabao 3-1 na Yanga.

Itakumbukwa kuwa bingwa wa michuano hiyo ndio atakayeiwakilisha Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani (2018), mashindano ambayo Azam FC atashiriki mwaka huu ikitarajia kumenyana na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mechi nyingine za ASFC;

Februari 24, 2017

Kagera Sugar v Stand United (Kaitaba Stadium, Bukoba)   

Mighty Elephant v Ndanda (Majimaji Stadium, Songea)

Madini v JKT Ruvu (Sheikh Amri Abeid Stadium, Arusha)

Februari 26, 2017

Mbao FC v Toto Africans (CCM Kirumba, Mwanza)

Tanzania Prisons v Mbeya City (Sokoine Stadium, Mbeya)

Simba v African Lyon (National Stadium, Dar es Salaam)

Yanga v Kiluvya (National Stadium, Dar es Salaam)