KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa mbinu za kiufundi walizobadilisha kipindi cha pili ndizo zilizochangia kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Azam Complex jana usiku.

Azam FC imeibuka kidedea kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) na kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 na timu hiyo katika mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.

Ushindi huo umezidi kuiweka kwenye hali mbaya ya kushuka daraja Ndanda, kwani mpaka hivi sasa ipo nafasi moja kutoka chini mkiani (15) ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 19 ikiizidi pointi tatu JKT Ruvu inayoburuta mkia kwa pointi zake 16.

Cheche ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wapinzani wao waliingia kwenye mchezo huo wakiwa wamepania kushinda ili kujinasua katika janga la kushuka daraja hali ambayo iliufanya mtanange huo kuwa mgumu.

“Mimi nafikiri kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia, lakini tulijaribu kufanyia marekebisho kwenye mapumziko kwa kuwataka wachezaji kuongeza spidi, wabadilike wanapotoka nyuma kuelekea mbele na kupiga mashuti kipindi cha pili, manake kipindi cha kwanza hatujapiga sana mashuti, hiyo imetusaidia kulitia hekaheka lango la wapinzani mpaka wamekuja kufanya makosa na sisi kupata bao,” alisema.

Kocha huyo aliendelea kufunguka kuwa, bado hawajakata tamaa kuelekea mbio za ubingwa, akidai wanachofanya hivi sasa ni kushinda mechi zao zote ili kuwapa presha waliojuu yake, Simba na Yanga.

“Hivi sasa tunahakikisha tunapambana kushinda mechi zetu zote, ili tuangalie yoyote anayefanya makosa lolote linaweza kutokea,” alisema.

Ushindi huo uliifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 37 na kubakisha pengo la pointi 12 baina yake na Yanga (49) iliyoko kileleni, Simba ni ya pili ikiwa nazo 48 Kagera Sugar inalingana pointi na matajiri hao katika nafasi ya nne lakini inazidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD).

Masoud ‘Cabaye’ kiwango

Akizungumzia kiwango cha kiungo kinda wa timu hiyo, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, aliyecheza kwenye kikosi cha kwanza kwenye mechi yake ya pili mfululizo jana ukijumlisha na ile ya Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns, Cheche alisema kwa kiasi kikubwa wameridhishwa na kiwango cha kinda huyo.

“Mimi nafikiri Masoud bado mchezaji kijana na mechi hizi mbili amecheza hakufanya vibaya amefanya vizuri sana, na sisi tunatimu zetu za vijana hapa tunajaribu kuwatangaza vijana wanaofanya vizuri, tumemjaribu kwenye mechi na Mamelodi amefanya vizuri, ili kumwongezea hali ya kujiamini lazima umpe mechi ya mwendelezo kidogo kidogo hadi atazoea kama walivyoanza wakina-Mudathir, ambao hivi sasa wanafanya vizuri,” alisema.