KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kushuka dimbani kuvaana  na Ndanda ya Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumapili saa 1.00 usiku.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na bonge la rekodi tokea mwaka huu uanze, kwani katika mechi tisa zilizopita za mashindano mbalimbali ilizocheza (sawa na dakika 810), matajiri hao wameruhusu wavu wao kuguswa mara moja tu.

Mechi hizo ni zile za ligi ilizoichapa Tanzania Prisons (1-0), Simba (1-0), sare dhidi ya Mbeya City, moto ulikolea zaidi ilipotwaa taji la Mapinduzi Cup bila kuruhusu bao ikiipiga Zimamoto (1-0), sare ilipocheza na Jamhuri (0-0), ikazigonga Yanga (4-0), Taifa Jang’ombe (1-0) na Simba (1-0).

Mchezo pekee ambao Azam FC imecheza mwaka huu na kuruhusu wavu wake kuguswa ni ule wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), ilipoichapa Cosmopolitan mabao 3-1.

Mbali na mechi hizo za mashindano, Jumatano iliyopita Azam FC ilicheza na Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki na kufanikiwa kuwabana vilivyo na kupelekea kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Ubora wa Azam FC hadi kufanikiwa kupata rekodi hiyo umetokana na uimara wa safu ya ulinzi ya timu hiyo chini ya kipa mahiri Aishi Manula na mabeki hodari wa kati, Yakubu Mohammed na Aggrey Morris, wanaosaidiwa na mabeki wa pembeni Gadiel Michael, Shomari Kapombe au Erasto Nyoni, huku wakipewa ulinzi mkali na viungo wakabaji Stephan Kingue, Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’ na Frank Domayo ‘Chumvi’.

Kuelekea mchezo huo, wachezaji wa Azam FC wamejipanga vilivyo kufanya kweli kwa kuibuka na ushindi kufuatia mafunzo makali wanayopewa na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba, Msaidizi wake Idd Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar.

Morali ya wachezaji wote waliokuwa fiti ipo juu kabisa kuhakikisha wanaipigania Azam FC kuondoka na pointi zote tatu, lakini itakuwa na pengo la wachezaji wake wanne waliokuwa wagonjwa ambao ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, viungo Stephan Kingue, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na beki wa kulia Shomari Kapombe.

Hadi timu hizo zinakutana, Azam FC ipo katika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 34, ikiwa nyuma ya pointi 15 na kinara Yanga aliyejikusanyia 49, Ndanda yenyewe ipo kwenye hatari ya kushuka daraja baada ya kujizolea pointi 19 ikiwa nafasi ya 15.

Rekodi zilipokutana (Head to Head)

Kihistoria kwenye mechi za ligi timu hizo zimekuwa na upinzani mkali, ambapo Azam FC imekutana na Ndanda mara tano na kushinda mechi mbili sawa na timu hiyo huku ikishuhudiwa mchezo mmoja ukiisha kwa sare.

Jumla ya mabao 10 yamefungwa kwenye mechi hizo tano (ukiwa ni wastani wa mabao mawili kila mechi), Azam FC ikiwa imefunga matano na Ndanda ikifanya kama hivyo kwenye wavu wa matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex.