MARA baada ya kucheza mchezo wake mkubwa ndani ya kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kiungo chipukizi Abdallah Masoud ‘Cabaye’ amemshukuru kocha wa timu hiyo kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza jana.

Cabaye jana alikuwa ni sehemu kikosi cha kwanza cha Azam FC kilichoanza kwa kucheza na Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns, kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuisha kwa sare ya bila kufungana.

Kiungo huyo aliyepandishwa msimu huu akitokea kwenye kituo cha kukuza vipaji cha timu hiyo ‘Azam FC Academy’, alionyesha uwezo mkubwa sana dhidi ya mabingwa hao hali ambayo ilimfanya kuwa kivutio kwa mashabiki na wengine hivi sasa kwenye mitandao ya kijamii wakianza kumuulizia alipotokea.

Licha ya nafasi yake ya kudumu kuwa eneo la kiungo, jana Kocha Mkuu Aristica Cioaba, alimwamini na kumpa majukumu ya kucheza nafasi ya winga ya kulia, nafasi ambayo alijitahidi kuimudu na kuwasumbua mno Mamelodi.

“Kwanza napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kumaliza mechi salama, halafu vilevile napenda kumshukuru kocha kwa kuniamini na kunipa nafasi leo, Mamelodi ni timu kubwa lakini kocha ameweza kunipa nafasi hii ni hatua nzuri kwangu katika kuendeleza kipaji changu,” alisema Masoud wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Masoud aliwaomba mashabiki wa timu hiyo waendelee kumwamini na kuisapoti Azam FC huku akiwaambia amejiandaa kuwapa mambo makubwa zaidi kuelekea mechi zijazo atakazopewa nafasi.

“Changamoto nyingi sana nimepitia kwenye mchezo huo, ukizingatia wenzetu wametuzidi baadhi ya vitu, hivyo nimejifunza vitu vingi kupitia mechi hiyo katika kuendeleza kipaji changu na kuisaidia timu yangu ya Azam FC, mashabiki wasichoke kunisapoti waendelee na naweza kuwaahidi mambo makubwa zaidi,” alimalizia Masoud.

Masoud ni moja ya matunda ya Azam Academy baada ya kulelewa vema tokea ajiunge na kituo hicho miaka kadhaa iliyopita akitokea Mtwara, na anaungana na mshambuliaji Shaaban Idd, ambao kwa pamoja wameanza kutazamwa kwa jicho la tatu katika kuongeza nguvu ndani ya timu kubwa wakitokea timu ya vijana.

Mbali na kukaa benchi kwenye baadhi ya mechi za Ligi Kuu msimu huu, Masoud alicheza mechi kadhaa za maandalizi ya msimu huu na kufunga bao moja maridadi la umbali wa mita 25 kwenye ushindi wa mabao 2-0 wa Azam FC dhidi ya Ashanti United.