KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku wa kuamkia leo imetoka sare tasa na Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sundowns ipo hapa nchini kwa kambi maalumu ya kujiandaa na mchezo wake wa Super Cup dhidi ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, TP Mazembe, utakaofanyika nchini Afrika Kusini Februari 18 mwaka huu.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake kutokana na ushindani mkubwa ulioonyeshwa na pande zote mbili, ilishuhudiwa kila upande ukikosa nafasi muhimu za kupata ushindi.

Washambuliaji wa Azam FC, Shaaban Idd na Yahaya Mohammed itabidi wajiulaumu wenyewe kutokana na kupoteza nafasi mbili za kuiweka mbele timu hiyo kwenye mchezo huo, Yahaya akipoteza mbili kipindi cha kwanza na moja kipindi cha pili.

Shaaban alifanya jitihada nzuri mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kuipenya ngome ya ulinzi ya Sundowns, lakini shuti alilopiga akiwa ndani ya eneo la 18 lilitoka sentimita chache ya lango.

Kiungo kinda wa Azam FC, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, aliyecheza mechi yake ya kwanza kubwa ndani ya kikosi hicho tokea apandishwe, aligeukia kivutio kwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri.

Wakati Sundowns ikibadilisha kikosi kizima dakika ya 60, Azam FC nayo kipindi cha pili iliwaingiza Enock Atta, Mudathir Yahya, Samuel Afful, Abdallah Kheri, Ramadhan Singano, mabadiliko ambayo yaliwaongezea kasi, lakini tatizo liliendelea kubakia katika eneo la ushambuliaji kwenye namna ya kuipenya safu ya ulinzi ya wapinzani wao.

Mara baada ya mchezo huo, Mamelodi itakipiga tena na African Lyon leo Alhamisi saa 1.00 usiku katika mchezo wa mwisho wa kirafiki nchini.

Azam FC ambayo itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho ikianzia raundi ya kwanza, imepata kipimo tosha kuelekea kuanza rasmi changamoto za kusaka hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wanatarajia kuanza changamoto ya michuano hiyo mwezi ujao (Machi), ikikutana na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali baina ya Orapa United ya Botswana au Mbabane Swallows ya Swaziland.