KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kukipiga na Mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, kwenye mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho Jumatano saa 1.00 usiku.

Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye mechi ya kirafiki, Agosti 7 mwaka 2013 zilikutana kwa mara ya kwanza jijini Johannesburg, Azam FC ilipoenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya na kuichapa timu hiyo bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa zamani, Gaudence Mwaikimba.

Kwa mujibu wa muandaaji wa ziara hiyo ya Mamelodi nchini, Rahim Kangezi Zamunda, amesema kuwa mchezo huo ni maalumu kwa ajili kampeni ya kupinga vita ujangili, iitwayo Linda Tembo Wetu. 

Mamelodi iliyokuja kuweka kambi hapa nchini, pia itautumia mchezo huo kama sehemu ya kupasha misuli kujiandaa na mchezo wa Super Cup dhidi ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika TP Mazembe, utakaopigwa Februari 18 mwaka huu.

Mara baada ya mchezo huo, Mamelodi itakipiga tena na African Lyon Alhamisi ijayo katika mchezo wa mwisho wa kirafiki nchini.

Azam FC ambayo itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho ikianzia raundi ya kwanza, hiko ni kipimo tosha kwa upande wao katika kuwapima wachezaji wake namna watakavyoanza changamoto za kusaka hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu, wanatarajia kuanza changamoto ya michuano hiyo mwezi Machi mwaka huu, ikikutana na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali baina ya Orapa United ya Botswana au Mbabane Swallows ya Swaziland.