BAADA ya kuichapa Simba bao 1-0 jana, Kocha Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, ametamba kuwa walikuwa na dawa ya kuimaliza timu hiyo huku akidai kwa sasa wamejidhatiti vilivyo kuirejesha Azam FC ile iliyotisha ambayo kila mtu alikuwa akiijua.

Bao pekee la Azam FC kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), liliwekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, aliyefikisha rekodi ya kuifunga Simba mabao 19 kwenye mechi za mashindano mbalimbali.

Cheche ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa haikuwa kazi rahisi kupata ushindi huo huku akidokeza kuwa waliingia kipindi cha kwanza kucheza kwa tahadhari kubwa na kukitumia kipindi cha pili kutumia udhaifu wa Simba na kupata bao hilo.

“Simba tayari tulicheza nayo mwanzo haijabadilika sana, mfumo wao waliocheza Unguja ndio ule ule ni sawa sawa na mgonjwa uliyeanza kumtibia umempa dawa karudi tena kwako unajua utampa dawa gani na matibabu yaendelee,” alisema.

Kocha huyo aliyeipa taji la Mapinduzi Cup timu hiyo wiki mbili zilizopita kwa kuifunga Simba bao 1-0, alisema kuwa wekundu hao waliingia kwenye mchezo huo wakitaka kujikomboa na ndio maana ilikuwa ngumu kwao kupata bao kipindi cha kwanza.

“Mimi namshukuru Mungu, nilisema mwanzo huko nyuma kuwa tunataka kuirudisha Azam FC yetu ambayo watu walikuwa wakiijua hapa kati tulipotea ni sehemu ya maisha kuna wakati unayumba, lakini sasa hivi tumeshaona wapi nini tufanye wapi tuelekee ili kuwarudishia ile hamu wachezaji watu na kufanya vizuri,” alisema.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC imefikisha jumla ya pointi 34 na kupanda hadi nafasi ya tatu ikilingana na Kagera Sugar lakini inaizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD), pia kwa sasa imebakisha pengo la pointi 12 kuifikia Yanga iliyo kileleni na 11 Simba iliyonafasi ya pili.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachochangamsha mwili na kuburudisha koo pamoja na Benki ya NMB, inatarajia kurejea mazoezini kesho jioni kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Ndanda utakofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi Ijayo saa 1.00 usiku.