KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kuizima Simba baada ya jioni ya leo kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Azam FC dhidi ya Simba mwaka huu, baada ya wiki mbili zilizopita kupata ushindi kama huo kwenye mchezo wa fainali wa Kombe la Mapinduzi na kulitwaa taji hilo.

Bao pekee la Azam FC limesukumizwa kimiani dakika ya 70 na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, aliyemzidi maarifa beki Method Mwanjali na kupiga shuti la chini lililomshinda kipa wa Simba, Daniel Agyei.

Hilo ni bao la nane kwa Bocco kwenye msimu huu wa ligi akizidiwa bao moja na wachezaji wa Yanga Amissi Tambwe, Simon Msuva na winga wa Simba, Shiza Kichuya, ambao wako kileleni wakiwa wamefunga mabao tisa kila mmoja.

Wakati huo huo, bao alilofunga Bocco leo limemfanya kuendeleza rekodi yake ya kuitesa Simba kwani hivi sasa ametimiza bao la 19 kuwafunga wekundu hao katika mechi za mashindano mbalimbali walizokutana.

Azam FC kama ingekuwa makini ingeweza kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa imefunga mabao mawili baada ya winga Joseph Mahundi na Bocco kushindwa kuzitumia nafasi zao nzuri mwanzoni mwa kipindi hicho.

Mshambuliaji Yahaya Mohammed, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ramadhan Singano ‘Messi, naye alikosa nafasi ya wazi dakika ya 68 akiwa na kipa baada ya kuchelewa kupiga mpira na kuporwa na Agyei miguu mwake.

Kwa ushindi huo, Azam FC hivi sasa imepunguza pengo la pointi baina yake na Simba iliyoko kileleni kwa pointi 45 na sasa kufikia 11, ikiwa imefikisha pointi 34 na kupanda hadi nafasi ya tatu ikilingana kwa pointi na Kagera Sugar lakini ikiizidi kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue/Mudathir Yahya, Himid Mao, Joseph Mahundi, Ramadhan Singano/Yahaya Mohammed dk 62, John Bocco (C)/Abdallah Kheri dk 83