MARA baada ya kuichakaza Cosmo Politan mabao 3-1 na kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Jumamosi ijayo itakuwa kibaruani kuvaana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.                        

Tayari kikosi cha Azam FC kimeanza rasmi mazoezi jana jioni kujiandaa na mtanange huo unaotarajiwa kuwa ni wa kisasi kwa pande zote mbili kutokana na aina ya matokeo yaliyotokea katika mechi zao za mwisho walizokutana msimu huu.

Wakati matajiri hao wa Azam Complex wakitaka kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, Simba nayo itataka kupooza machungu ya kufungwa na Azam FC kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi (1-0) wiki moja na nusu iliyopita.

Kuelekea mchezo huo, manahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ na Shomari Kapombe, wametoa neno kwa upande wa wachezaji wenzao namna walivyojithatiti kuibuka na pointi zote tatu dhidi ya wapinzani wao hao.

Bocco alisema kuwa mchezo huo hautakuwa rahisi bali utakuwa mgumu, lakini watajituma na kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

“Tukikutana na Simba tunakuwa tunacheza mpira wa kujuana na pia wa kuogopana, lakini naamini ni mechi ngumu, watakuwa na mipango yao na sisi tutajipanga kwa upande wetu, naamini tutajituma na tutaweza kupata ushindi,” alisema nyota huyo.

Bocco ataingia kwenye mchezo huo akiwa na rekodi ya aina yake ya kuifunga mabao mengi Simba kuliko mchezaji mwingine yoyote kihistoria, akiwa tayari ameshaziona nyavu zao mara 18 katika mechi za mashindano mbalimbali.

Kapombe ambaye ni mmoja wa manahodha wasaidizi wa Azam FC, naye alisema kuwa wanaendelea kujipanga vema na kufanya maandalizi kuelekea mchezo huo ili kupata ushindi.

“Jumamosi tuna mechi kubwa na mechi ngumu kwa sababu Simba hivi sasa ndio vinara wa ligi, ni timu nzuri tumeshakutana nayo Zanzibar tumeweza kupata ushindi, hivi sasa tumejipanga vizuri na tunaendelea kufanya maandalizi ili tuweze kupata ushindi kama tulivyofanya mechi iliyopita,” alisema.

Bao pekee la Azam FC kwenye mchezo huo uliofanyika Zanzibar, lilifungwa kiufundi na nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, aliyefunga kwa shuti kali la umbali wa mita 30 na kuihakikishia timu hiyo kutwaa taji la pili la msimu baada ya mwanzoni mwa msimu kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuichapa Yanga.

Timu hizo zinakutana wakati Azam FC ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 31 ikizidiwa pointi 14 na Simba iliyojikusanyia 45 kileleni, Yanga ni ya pili ikiwa nazo 43 huku Kagera Sugar iliyocheza mchezo mmoja zaidi ikikamata ya tatu ikiwa nazo 34.