MABAO matatu yaliyofungwa na nahodha John Bocco, Shaaban Idd na Joseph Mahundi, yametosha kabisa kuivusha Azam FC kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) ikiichapa Cosmo Politan 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC iliuanza mchezo huo kwa kasi katika dakika 15 za kwanza za mchezo huo, lakini ilishindwa kuipenya safu ya ulinzi ya Cosmo kufuatia eneo la ushambuliaji na kiungo kutoelewana vizuri.

Dakika ya 16 Bocco alikaribia kuipatia bao la uongozi Azam FC, lakini kichwa cha chini alichopiga kilitoka sentimita chache ya lango la Cosmo Politan, dakika 15 baadaye Yahaya Mohammed, naye alikosa nafasi ya wazi akiwa ndani ya eneo la 18 baada ya mpira aliopiga kupaa juu ya lango.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, timu zote zilienda mapumziko zikiwa hazijafungana, Azam FC ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili ikiwatoa kiungo Frank Domayo na Yahaya na kuwaingiza Joseph Mahundi na Shaaban Idd.

Mabadiliko hayo yaliongeza kasi kwa upande wa Azam FC kutokana na kuongeza presha langoni mwa Cosmo, ambapo dakika ya 49 Shaaban alimiliki vema mpira ndani ya eneo la 18 mbele ya mbele ya mabeki lakini shuti alilopiga lilimlenga kipa wa Cosmo.

Dakika ya 69 Bocco aliwanyanyua vitini mashabiki wa Azam FC baada ya kutumia uzembe wa kipa wa Cosmo aliyeupiga mpira uliombabatiza kwenye kisigino na kujaa wavuni.

Bocco hakushangilia bao hilo kama alivyoahidi kabla ya mchezo huo kutokana na timu hiyo kuwa ndiyo iliyomlea na kumtoa kabla ya kusajiliwa na Azam FC.

Shaaban aliifungia bao la pili Azam FC dakika ya 76 akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Cosmo kufuatia shuti alilopigiwa na Bocco. Mahundi alipigilia msumari wa mwisho langoni mwa timu hiyo dakika ya 80 baada ya kupiga shuti kali lililojaa wavuni akiwa ndani eneo la 18.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika, Azam FC iliondoka uwanjani na ushindi huo mnono na sasa inasubiria kupangiwa mpinzani wake atakayepambana naye katika hatua ya 16 bora.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Jumamosi ijayo kupambana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodadom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue/Singano dk 73, Himid Mao, Salum Abubakar, Frank Domayo/Mahundi dk 45, John Bocco (C), Yahaya Mohammed/Shaaban dk 45