KWA mara ya kwanza mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC, tokea watoke visiwani Zanzibar kutwaa taji hilo, watashuka dimbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kukipiga na Mbeya City leo saa 1.00 usiku.

Kwa upande wa mashabiki, kama ulikosa fursa ya kuiona Azam FC moja kwa moja uwanjani wakati ikishiriki michuano hiyo na kutwaa taji, sasa kazi ni kwenu kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu na kuwashuhudia mabingwa hao ikiwemo kuwapongeza wachezaji kwa kazi nzuri waliyoifanya Zanzibar.

Kujitokeza kwenu kwa wingi kutazidi kuwapa hamasa wachezaji, hali ambayo itawapa nguvu zaidi na hatimaye kuendeleza mazuri ya visiwani Zanzibar. Tiketi za mchezo huo zinapatikana kwa bei chee tu, Sh. 3,000/= kwa mzunguko na Sh. 10,000/= kwa viti vya watu maalumu (V.I.P).

Unaachaje kuwaona mabingwa wa Mapinduzi? Toroka uje Azam Complex uone wakionyesha uhondo na burudani ya aina yake bila kukosa yale mashuti ya mbali yaliyopachikwa jina la ‘Mama Mkanye Mwanao’.

Kikosi cha Azam FC kitaingia kwenye mchezo huo kikiwa na morali kubwa na ari nzuri kutokana na ubingwa wa Mapinduzi Cup walioutwaa kwa kuweka rekodi mpya ya kutofungwa mechi wala kuruhusu bao katika mechi tano walizocheza za michuano hiyo.

Kwa kukiongezea nguvu zaidi kikosi chake, tayari Kocha Mkuu mpya raia wa Romania, Aristica Cioaba, ameshaanza kazi rasmi akiwa na usaidizi wa makocha wazawa, Idd Nassor Cheche aliyeipa Azam FC taji hilo na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar.

Wachezaji wameonekana kuyafurahia mazoezi ya kocha mpya na kuyaelewa haraka, hali ambayo imezidi kuleta taswira nzuri kuelekea mchezo huo, ambao ni muhimu kwa upande wa Azam FC kushinda ili kuongeza zaidi morali kikosini na kuendeleza moto waliotoka nao Zanzibar.

Kwa mara ya kwanza winga Joseph Mahundi, aliyesajiliwa na Azam FC akitokea Mbeya City kwa usajili huru, ataingia uwanjani kupambana dhidi ya timu yake ya zamani, sambamba na winga Mrisho Ngassa anayekipiga huko hivi sasa, naye atashuka dimbani kuvaana na Azam FC aliyowahi kuichezea miaka michache iliyopita iliyomsajili akitokea Yanga kabla ya kumtema kwa vitendo vya utovu wa nidhamu.

Taarifa za kikosi

Kuelekea mchezo huo Azam FC itawakosa wachezaji wake wawili; beki wa kushoto, Bruce Kangwa, aliyeko nchini Gabon kwenye kikosi cha timu yake ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’, kinachoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) pamoja na winga Khamis Mcha ‘Vialli’, anayesumbuliwa na maumivu ya nyonga.

Msimamo unasemaje

Hadi timu hizo zinaelekea kucheza mechi za raundi ya 19, Azam FC imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 30 katika nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kushinda mechi nane, sare sita na kufungwa mara nne, ambapo inazidiwa pointi 14 na Simba iliyoko kileleni.

Mbeya City yenyewe ipo nafasi ya saba kwenye msimamo baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 24 zilizotokana na kushinda mechi sita, sare sita na kufungwa michezo sita.

Rekodi zilipokutana (Head to Head)

Kihistoria tokea Mbeya City icheze kwenye ligi kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14, timu hizo zimekutana mara saba katika ligi hiyo, huku rekodi ikionyesha kuwa timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya haijawahi kuifunga Azam FC katika mchezo wowote.

Katika mechi hizo, Azam FC imeshinda mara tano na ikishuhudiwa mechi mbili zikiisha kwa sare, zote zikipigwa Uwanja wa Azam Complex huku sare ya kukumbukwa zaidi ni ile ya mabao 3-3.

Mbali na historia hiyo, itakumbukwa kuwa Aprili 13, 2014, mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) waliandika rekodi ya kutwaa taji la ligi kwa mara ya kwanza pale walipoichapa Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, mabao yaliyofungwa na Gaudence Mwaikimba na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyetupia la ushindi.  

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye ligi ilikuwa ni Septemba 10 mwaka jana jijini Mbeya, ambapo Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-1 yaliyowekwa kimiani na mawinga Khamis Mcha na Gonazo Ya Thomas, ambaye hayumo kikosini baada ya kusitishiwa mkataba, bao la Mbeya City lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Rafael Alpha.