KIKOSI kazi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimewasili jioni ya leo jijini Dar es Salaam mara baada ya usiku wa jana kutwaa taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Azam FC imetwaa taji hilo la tatu kihistoria kwa kuweka rekodi ya aina yake, baada ya kutofungwa mchezo wowote wala kuruhusu bao katika mechi tano ilizocheza za michuano hiyo, ikivifunga vigogo vya Tanzania, Simba (1-0) na Yanga (4-0), ikatoa dozi pia kwa Zimamoto (1-0), Taifa ya Jang’ombe (1-0), huku ikipata suluhu dhidi ya Jamhuri.

Mara baada ya mchezo huo wa fainali, wachezaji na viongozi wa Azam FC walipata fursa ya kuzungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz na kuelezea hisia zao kwa namna walivyoupokea ubingwa huo.

Kocha Cheche

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, aliyeiongoza timu hiyo kwenye michuano hiyo alisema kuwa jambo kubwa lilipelekea mafanikio hayo kwa kikosi chake ni mshikamano, hali ya kujituma kwa wachezaji na kufuata maelekezo yake.

“Unajua unapokuwa binadamu na ukapata mafanikio makubwa kama haya ndani ya muda mfupi lazima uwe na furaha, nawashukuru wachezaji wangu kwa kzi kubwa waliyofanya na mshikamano na hali ya kujituma na jitihada walizozionyesha, kwa hakika hivyo ndivyo vilivyotupa ubingwa,” alisema.

Cheche alisema moto huo waliouwasha ni wa tipa (ule wa kwenye viwanda vya mafuta) na hauwezi kuzimika huku akidai kuwa wanatarajia kuuhamishia kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), wanazotarajia kuanza kucheza kuanzia wiki ijayo.

Kocha huyo aliyekuwa akisaidiana na Kocha wa Makipa Idd Abubakar, kufanya kazi hiyo kubwa hadi kufikia mafanikio hayo, kuanzia kwenye ligi watakuwa chini ya Kocha Mkuu mpya, Mromania Aristica Cioaba, aliyechukua mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez, aliyesitishiwa mkataba pamoja na benchi lake zima la ufundi.

Nahodha Bocco

Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, alisema kuwa wanafuraha kubwa kutwaa taji hilo huku akiwapongeza wachezaji wenzake kwa namna walivyojituma hadi kufikia fainali na kupata mafanikio hayo.

“Kwanza tunamshukuru Mungu kwa ushindi huu ni matokeo mazuri kwetu tumeweza kutwaa Kombe la Mapinduzi, kikubwa nawaomba wachezaji wenzangu tuweze kuweka jitihada katika michezo ya Ligi Kuu ianyokuja, tuwasikilize walimu wetu nini wanachotueleza ili tuweze kufanya vizuri na hata michuano ya kimataifa,” alisema.

Bocco alieleza siri ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo, akidai kuwa: “Naamini hatukuwa na papara, tuliweza kutulia, tuliweza kupata sapoti kutoka kwa viongozi wetu pamoja na mashabiki wetu na kuwasikiliza walimu wetu ndio kama hivi tunamshukuru Mungu tumeanza kidogo kupata mafanikio.”

Kapombe

Beki wa kulia wa Azam FC, Shomari Kapombe, alisema: “Mimi najisikia furaha kutokana na namna tulivyocheza, mara ya kwanza tulianza taratibu sana na mwisho wa siku tukakaa kwenye fomu yetu na kushinda na kuwa mabingwa, lakini kubwa ninalofurahia zaidi ni sisi kutoruhusu bao lolote, hiyo ndiyo furaha yangu mimi kama beki.”

Kapombe alifichua siri ya wao kama safu ya ulinzi kumaliza michuano hiyo bila kuruhusu bao lolote, ambapo amesema kuwa hiyo imetokana na tabia ya kuhamasishana kutofungwa bao waliyokuwa nayo, kwa mabeki wanaocheza uwanjani na hata wale wanaokuwa benchi.

“Eneo letu lote la ulinzi kwa wachezaji wanaokaa nje na sisi tunaocheza, huwa siku zote tunahamasishana kila tunapoingia kwenye mechi, tuweze kufanya vizuri na kumaliza mechi bila kufungwa na kweli tumefanikiwa tumecheza michuano yote bila kufungwa, hii ni hongera kwetu sisi na wachezaji wote wanaocheza eneo la ulinzi.” alisema.

Katika hatua nyingine, aliwapongeza mashabiki wa Azam FC waliosafiri na kwenda kuwasapoti, huku akiwaambia kuwa: “Mimi napenda kuwaambia wasikate tamaa, waendelee kuisapoti timu yao popote inapokwenda ili tuweze kupata ushindi na kuwapa furaha.”

Aggrey

Mchezaji bora wa mchezo huo wa fainali, beki wa Azam FC Aggrey Morris, alisema kuwa ubingwa walioupata ni kama motisha kwa upande wao kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri kwenye ligi, huku akidai kuwa moto huo wataendelea nao kwenye ligi ili kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri.

“Nashukuru kwa kuwa mchezaji bora wa mechi, ila mechi tumecheza watu wengi lakini kuchaguliwa mchezaji bora kwangu ni furaha kwa sababu kila mchezaji akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi basi anajisikia furaha, lakini huu ushindi wangu si kwangu pekee bali ni kwa timu nzima,” alisema.

Aishi  

Kipa bora wa michuano hiyo, Aishi Manula, ambaye amecheza mechi zote bila kufungwa bao, amesema anajisikia faraja sana kuweza kutwaa tuzo hiyo huku akiwaambia mashabiki kuwa ubingwa huo unaamanisha kuwa wao wamerudi kwenye ubora wao na kuonyesha kama ni timu kubwa.

“Napenda kumshukuru Mungu, kwa hiki ambacho wamenipatia na pia kuishukuru timu nzima kwa ujumla kwa kuweza kucheza vizuri hasa mabeki wameweza kunilinda vizuri na tumeweza kumaliza mashindano haya bila kuruhusu bao, pia ni kitu kizuri kwa sababu hili linakuwa kombe la pili kuchukua bila kuruhusu bao, kwanza Kagame tuliweza kulichukua bila kuruhusu bao na hili la Mapinduzi kwa hiyo ni kitu kizuri,” alisema.

Mwenyekiti atoa neno

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Azam FC, Idrissa Nassor ‘Father’, alisema kuwa anashukuru Mungu kwa timu yake hiyo kuweza kutwaa taji la michuano hiyo iliyoshirikisha timu kubwa.

“Kwetu hii ni furaha kubwa mimi na vijana wangu na viongozi wenzangu na mashabiki wetu, nawaambia mashabiki waendelee kutusapoti kwenye mchezo wa mpira mashabiki ni sehemu muhimu sana kwa sababu mashabiki nao wanasehemu yao kuhamasisha ushindi, wachezaji wanacheza, viongozi wanahangaika na wao wanahamasisha ushindi, nasisitiza wazidi kutuunga mkono ili tuweze kufika kule tunapotaka kwenda,” alisema.

Ofisa Mtendaji anena

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alifurahishwa na namna timu hiyo ilivyotwaa taji hilo kwa kuandika rekodi ya kutofungwa bao huku akidai kuwa hiyo ni chachu nzuri ya kwenda kufanya vizuri kwenye ligi.

“Tunawapongeza sana wachezaji wetu, tunawapongeza sana bodi ya Wakurugenzi wote wa kampuni yetu ambao ndio wadhamini mama wa timu yetu, washamini wetu wakuu Benki ya NMB, wote tunawapongeza kwa kuweza kutupa sapoti, kikubwa kabisa ni wachezaji wetu na benchi la ufundi wameweza kufanya kitu ambacho wengi hawakutarajia, hili ni taji letu la pili kwa msimu huu baada ya kutwaa Ngao ya Jamii Agosti mwaka jana.

“Kwa hiyo mipango yetu kama klabu tunaona inaelekea vizuri, ligi hatupo nafasi nzuri lakini kwa ushindi huu ni chachu ya kwenda kwenye ligi na kujipanga vizuri, kwa hiyo hivi sasa tuna ligi, FA Cup na Kombe la Shirikisho Afrika, makombe matatu bado yako njiani, tumechukua mawili kwa hiyo hayo matatu pia tunaweza kuyapata, jambo muhimu ni umoja wetu, ushirikiano, wapenzi wetu wa mpira waendelee kutusapoti,” alisema.

Kawemba alisema kuwa anaimani kubwa wakipata sapoti yao na kutoka kwa Wakurugenzi wa bodi, wadhamini na mashabiki wao, wataweza kutwaa makombe hayo matatu yaliyobakia na hatimaye kumaliza msimu kwa staili ya aina yake.

Muendelezo VPL   

Mara baada ya Azam FC kurejea, kesho Jumapili jioni inatarajia kuingia kambini na kuanda mazoezi saa 1.00 usiku kujiandaa na mchezo wa ujao wa ligi dhidi ya Mbeya City utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatano ijayo saa 1.00 usiku.