NI raha tu! Hiyo ni baada ya Azam FC muda mchache uliopita kuendeleza dozi kwenye Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa Taifa ya Jang’ombe bao 1-0 na kutinga fainali ya michuano hiyo itakayofanyika Januari 13 mwaka huu.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa baada ya kutoka kuifunga Yanga mabao 4-0, na mara baada ya kufika hatua hiyo hivi sasa inamsubiria mshindi wa nusu fainali ya pili itakayowakutanisha Yanga na Simba saa 2.15 usiku.

Hiyo ni fainali ya tatu kuingia Azam FC kwenye michuano hiyo, mara mbili zilizopita ilikuwa mwaka 2012 na 2013 ambapo iliweza kulitwaa taji hilo mfululizo na kuandika rekodi ya kuwa timu pekee kuwahi kufanya hivyo.

Bao pekee la Azam FC limefungwa na kiungo Frank Domayo, dakika ya 33 akilifunga kwa ufundi mkubwa baada ya kufumua shuti kali nje ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Jang’ombe.

Kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kwenye mtanange huo, jopo la makocha lilimchagua kiungo huyo kuwa Mchezaji Bora wa mchezo na kukabidhiwa katoni nne za kinywaji safi kilichokuja na muonekano mpya, Azam Malti pamoja na kiatu cha kuchezea mpira.

Mchezo huo ulishuhudiwa jukwaani na Kocha Mkuu mpya wa Azam FC raia wa Romania, Aristica Cioaba, ambaye tayari amesaini mkataba wa miezi sita wenye kipengele cha kuongezwa mwishoni mwa msimu kulingana na mafanikio atakayoipatia timu hiyo.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) na Ngao ya Jamii, wametinga fainali ya michuano hiyo wakiwa na rekodi ya aina yake kwani ndio timu pekee ambayo haijafungwa bao lolote mpaka sasa ndani ya mechi nne ilizocheza ikiwa imefunga mabao sita.

Kikosi kilichocheza leo:

Aishi Manula, Shomari Kapombe/Himid Mao, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue/Abdallah Kheri dk 79, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco (C), Yahaya Mohammed/Shaaban Idd dk 59, Joseph Mahundi/Enock Atta Agyei dk 75