IMEFAHAMIKA! Ndivyo unavyoweza kusema hivyo, baada ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, muda mchache uliopita kumjua mpinzani wake atayecheza naye kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi ambaye ni timu ya Taifa Jang’ombe.

Jang’ombe inakutana na Azam FC katika mchezo huo utakofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar keshokutwa Jumanne saa 10.15 jioni, baada ya kumvua taji bingwa mtetezi wa michuano hiyo, URA ya Uganda kwa kuifunga bao 1-0 katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi A.

Azam FC inakutana na timu hiyo ikiwa na morali kubwa baada ya jana kuipa kisago kikali cha mabao 4-0 Yanga katika mchezo wa mwisho wa Kundi B, ambao uliwafanya matajiri hao kupanda kileleni mwa kundi hilo ikifikisha pointi saba, Yanga ikifuatia kwa pointi zake sita, Zimamoto (3) na Jamhuri (1).

Mara ya mwisho Azam FC kukipiga na Jang’ombe ilikuwa ni Julai 31 mwaka jana kwenye mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu huu, ambapo mabingwa hao wa Ngao ya Jamii walishinda bao 1-0 lililowekwa kimiani kiufundi na mshambuliaji aliyekuwa katika majaribio Mburundi Fuadi Ndayisenga.

Wakati Azam FC ikisaka fainali ya michuano hiyo itakayofanyika Januari 13, mtanange mwingine wa kukata na shoka unatarajia kuwahusisha mahasimu wa jiji la Dar es Salaam, Simba na Yanga ambazo zitakutana katika nusu fainali ya pili itakayofuatia itakayopigwa siku hiyo saa 2.15 usiku.

Azam FC ikifanikiwa kutinga hatua ya fainali huenda ikakutana tena na Yanga iliyokutana naye hatua ya makundi au Simba, zote zikitarajia kuwa mechi kubwa zinazovuta hisia za mashabiki wengi wa soka nchini na baadhi ya maeneo la Afrika Mashariki.