BAADA ya jana kuiongoza Azam FC kuichapa Yanga mabao 4-0 kwenye Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa muda wa kikosi hicho, Idd Nassor Cheche, amewaambia mashabiki wa timu hiyo wakae mkao wa kufurahi zaidi huku akiwataka wasubirie taji hilo jijini Dar es Salaam.

Cheche ameendeleza rekodi nzuri tokea akabidhiwe mikoba ya Wahispania waliositishiwa mikataba wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hetnandez, ambapo mabao hayo muhimu ya Azam FC jana yalifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Yahaya Mohammed, Joseph Mahundi ‘Benteke’ na Enock Atta Agyei.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Cheche alisema kuwa haikuwa kazi rahisi kuwafunga idadi hiyo ya mabao wapinzani wao na kudai kuwa iliwachukua muda mrefu kuweza kuvunja nguvu zao na kupata matokeo waliyoyapata.

“Mchezo ulikuwa mzuri tokea mwanzo, wapinzani wetu hawakuwa rahisi, kama ulivyoona ilituchukua muda mrefu kupata mabao mengine tokea tulipofunga la kwanza, mipango yetu tuliyopanga toka mwanzo kuelekea mechi hii iliweza kufanya kazi na wachezaji kuifanyia kazi vizuri na ikatuletea matokeo,” alisema.

Siri tatu za ushindi

Kocha huyo wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Azam FC, alitaja siri tatu zilizochangia timu hiyo kupata ushindi huo mnono, ambao ni mkubwa kihistoria tokeo timu hizo zilipoanza kukutana.

“Ushindi wetu umetokana na mshikamano kwanza, nidhamu ya wachezaji nay ale matatizo tuliyokuwa nayo kuyafanyia kazi na wachezaji wameyapokea vizuri na vyote hivyo vimetuletea matokeo.

Changamoto nusu fainali

Kuelekea changamoto ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo Azam FC tayari imeshafuzu, Cheche alisema kuwa kikosi chake kitakuwa moto zaidi kuelekea hatua hiyo.

“Tulivyoanza na kadiri tunavyoelekea mbele zaidi na kuyafanyia kazi mapungufu na wachezaji kuwa wasikivu, wananisikiliza, wanafuata maelekezo, mimi nafikiri tutafanya mambo makubwa zaidi ya haya tuliyofanya,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola na Benki ya NMB, kwa sasa inasubiria kujua mpinzani wake atakayekutana naye kwenye hatua ya nusu fainali, ambaye anatokea Kundi A, kati ya Simba, URA, Jang’ombe Boys na Taifa ya Jang’ombe.

Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, ikifanikiwa kutwaa taji hilo itakuwa ni mara yake ya tatu kufanya hivyo baada ya kulibeba mara mbili mfululizo mwaka 2012 na 2013 na kuwa timu pekee iliyolitwaa mfululizo kihistoria.