HUKU ikicheza soka la hali ya juu, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC usiku huu imeiendesha mchakamchaka Yanga kwa kuigonga kipigo kizito cha mabao 4-0 kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Aina ya ushindi iliyoupata Azam FC na kasi iliyoonyesha mchezoni, ilitosha kabisa kwa mashabiki kuifananisha timu hiyo na ile kasi ya juu ya mtandao wa ‘intaneti’ ya 4G.

Iliichukua Azam FC dakika ya pili kuandika bao la kwanza lilifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ kwa shuti akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’, kufuatia kupangua shuti lililopigwa na Joseph Mahundi.

Azam FC iliendeleza kasi ya mshambulizi, ambapo dakika ya 23 ilifanya shambulizi jingine kali langoni mwa Yanga, lakini shuti lililopigwa na kiungo mkabaji Stephan Kingue, lilitoka sentimita chache ya lango.

Dakika ya 41 Bocco alikaribia kuipatia bao la pili Azam FC baada ya kuwatoka mabeki kadhaa wa Yanga na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa na kukosa mmaliziaji kabla ya kuwaahi tena na kuudaka.

Mchezaji bora wa mchezo huo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, dakika ya 43 aliwatoka mabeki watatu wa Yanga na kuingia kwenye eneo la 18 lakini shuti alilopiga lilimbabatiza beki kabla ya mpira kuokolewa.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa bao hilo ambapo ilirejea tena makali kipindi cha pili na kufanya mashambulizi kadhaa mwanzoni mwa kipindi hicho.

Shambulizi kali lililofanywa kuelekea langoni mwa Yanga dakika ya 54 lilizaa matunda baada ya Yahaya Mohammed kuipatia bao la pili Azam FC kwa kichwa akimalizia krosi safi iliyochongwa na Sure Boy.

Winga Mahundi ambaye naye aliendeleza kiwango chake bora dakika ya 80 alifunga bao zuri la umbali wa takribani mita 25 na kuipa uongozi wa mabao 3-0 Azam FC.

Mabadiliko yaliyofanywa na Azam FC dakika ya 79 ya kuingia winga Enock Atta Agyei na kutoka kiungo Frank Domayo, yalizidi kuitakatisha timu hiyo baada ya Enock kuifungia bao la nne dakika ya 84 akimalizia pasi safi ya Samuel Afful ambaye naye aliingia dakika ya 65 kuchukua mikoba ya Yahaya aliyeumia.

Kuelekea dakika za mwisho, Azam FC ingeweza kupata bao la tano na sita kama Sure Boy na Afful wangeweza kuzitumia vema nafasi walizopata.

Kama kawaida mchezaji bora wa mchezo huo, Sure Boy, alikabishiwa katoni nne za kinywaji safi kisicho na kilevi cha Azam Malti huku timu zote mbili nazo zikipewa idadi hiyo ya katoni kila mmoja.

Ushindi huo mnono unaifanya Azam FC kumaliza hatua ya makundi ya michuano hiyo ikiwa kileleni mwa Kundi B baada ya kufikisha pointi saba, Yanga ikifuatia wakiwa nazo sita, Zimamoto (3) na Jamhuri (1).

Azam FC, Bocco rekodi

Ushindi huo umeiongezea rekodi Azam FC katika mechi za mashindano mbalimbali walizokutana na Yanga, ambapo hivi sasa rekodi inasomeka kuwa katika mechi 28 walizokutana kila timu imeshinda mara 10, sare nane, huku matajiri hao wakiwa wamefunga mabao mengi zaidi, 38 na Yanga 37.

Bao alilofunga Bocco linamfanya kutimiza mabao 13 aliyoifunga Yanga kihistoria akiwa ni mchezaji pekee aliyeifunga mabao mengine timu hiyo pamoja na Simba, ambayo nayo ameitupia wavuni mara 18.  

Mwaka 2012 Azam FC ilipotwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza, iliifunga Yanga mabao 3-0 na kuiondosha mashindanoni timu hiyo, safari hii ushindi unaifanya iandike rekodi ya kuipa kipigo kizito Yanga kihistoria.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Yakubu Mohammed/Abdallah Kheri dk 90, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo/Enock Atta dk 79, John Bocco (C)/Mudathir Yahya dk 86, Yahaya Mohammed/Samuel Afful dk 65, Joseph Mahundi