KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumamosi itakuwa kibaruani kuhakikisha inasonga kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi pale itakapokuwa ikivaana na Yanga.

Mtanange huo wa kukata na shoka unaotawaliwaga na upinzani mkali kwa pande zote mbili, unatarajia kuanza saa 2.15 usiku ndani ya Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Azam FC tayari imeshatanguliza mguu mmoja kuelekea hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, baada ya kujikusanyia jumla ya pointi nne kufuatia kushinda mchezo mmoja na sare moja.

Wakati timu zote zikiwa zimebakisha mechi moja za mwisho za hatua ya makundi, msimamo wa Kundi B mpaka sasa unaonyesha kuwa Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi sita, inafuatiwa na Azam FC iliyojikusanyia nne, Jamhuri ipo nafasi ya tatu baada ya kujizolea moja huku Zimamoto ikifunga dimba kufuatia kutokuwa na pointi hata moja.

Kuelekea mchezo huo dhidi ya Wanajangwani hao, zifuatazo ni sababu muhimu ambazo zinaipa nafasi kubwa Azam FC kutanguliza mguu wa pili kwa kutinga hatua hiyo;

Haijafungwa bao

Azam FC iliyofunga bao moja mpaka sasa, ni miongoni mwa timu mbili zenye safu ngumu ya ulinzi baada ya kutoruhusu kufungwa bao lolote, nyingine ikiwa ni Yanga, zote zikiwa ni timu kutoka Kundi B.

Rekodi hiyo inaibeba Azam FC kuelekea vita ya kuwania nafasi moja iliyobakia kwa timu kutoka kundi hilo kutinga kwa hatua ya nusu fainali, hiyo inatokana na mpinzani wake Jamhuri kufungwa mabao mengi.

Mpaka sasa Jamhuri ikielekea kufunga dimba kwa kucheza na Zimamoto, imeruhusu wavu wake kutikiswa mara sita huku ikiwa haijafunga bao lolote.

Hesabu hazimbebi mpinzani

Hata kama Azam FC ikipoteza mchezo wa mwisho, ili Jamhuri iweze kusonga mbele itatakiwa imfunge Zimamoto kuanzia mabao saba bila kuruhusu bao, jambo ambalo ni gumu kwa upande wao.

Hesabu muhimu Azam FC

Azam FC bado ina uchaguzi wa matokeo mawili ya kuyapata kesho ili iweze kusonga mbele; Matokeo ya sare yoyote au ushindi bado yataihakikishia nafasi hiyo mabingwa hao wa Ngao ya Jamii. Ushindi utaifanya pia kumaliza kama kinara wa kundi hilo kwani watakuwa wamefikisha pointi saba huku ikiiacha Yanga kwenye nafasi ya pili kwa pointi zao sita.

Kauli kocha, nahodha

Kocha Mkuu wa muda wa Azam FC, Nassor Idd Cheche, amesema kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wamejipanga kufanya vizuri.

“Katika mchezo wetu uliopita (Jamhuri), tulifanikiwa kumiliki mpira kwa asilimia 80, lakini tatizo lilikuwa ni umaliziaji kwenye eneo la ushambuliaji, nimeshalifanyia kazi suala hilo kwenye mazoezi, naamini italeta tija kesho tutakapocheza dhidi ya Yanga.

“Mechi haitakuwa rahisi, itakuwa ngumu lakini sisi na Yanga mara nyingi tumecheza wakati mwingine tunawafunga na wanatufunga na tunafungana, mchezo utakuwa mzuri nafikiri kwa mazoezi tuliyoyafanya na marekebisho tunawaahidi mashabiki tutafanya vizuri,” alisema.

Naye Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, alisema kuwa kwa namna anavyowaona wachezaji wenzake wakiwa kwenye ari nzuri na morali mazoezini, anaamini hiyo ni dalili nzuri ya kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Wachezaji wako katika ari nzuri, cha muhimu zaidi ni katika mazoezi mjitahidi kuwa kwenye ari nzuri yaani muwe na nguvu, muwe na furaha, kwa hiyo kinachofuatia ni mechi, tutajitahidi kufanya vizuri zaidi katika mchezo huo,” alisema

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo ilikuwa ni mwaka jana katika hatua kama hii ya makundi, ambapo ilishuhudiwa mtanange huo ukiisha kwa sare ya bao 1-1, Kipre Tchetche akitangulia kuifungia Azam FC kabla ya Vicent Bossou kuisawazishia Yanga.

Bao hilo la Yanga lilizua utata mkubwa baada ya mpira kuonekana haujavuka mstari wa lango kufuatia kiungo Mudathir Yahya kuokoa kwenye mstari mpira uliopigwa na Bossou.

Awali ya hapo timu hizo ziliwahi kukutana pia katika hatua hiyo mwaka 2012 na kushuhudiwa Azam FC ikitakata vilivyo kwa kuicharaza Yanga mabao 3-0 na kuitupa nje ya michuano hiyo.