BAADA ya kutokuwa kwenye kiwango chake kwenye mechi mbili zilizopita, winga wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Enock Atta Agyei, amepanga kuwashangaza mashabiki wa timu hiyo kwenye mchezo wa keshokutwa Jumamosi dhidi ya Yanga.

Mchezo huo wa mwisho wa Kundi B la michuano ya Kombe la Mapinduzi unatarajia kufanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15 usiku.

Agyei ambaye anakipaji cha hali ya juu cha kuuchezea mpira, ameshafanikiwa kuichezea Azam FC mechi mbili za mashindano (Zimamoto, Jamhuri) tokea alipojiunga nayo msimu huu akitokea Medeama ya Ghana.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz nyota huyo aliyetimiza umri wa miaka 18 leo, alisema kuwa bado hajafanikiwa kucheza vema kama wengi walivyotarajia kwenye mechi mbili hizo alizocheza.

“Ninawaahidi mashabiki wa Azam FC mambo mazuri, japo mchezo wangu wa kwanza na wa pili huku, sikucheza kama walivyotarajia, nazidi kuomba mambo yaende sawa kama inavyotakiwa, katika mechi ya Jumamosi (Yanga) ambayo tutacheza nitawashangaza, hicho nawaahidi,” alisema.

Katika hatua nyingine, alifurahia kuongeza mwaka mmoja leo katika siku yake ya kuzaliwa huku akisema kuwa anafurahia sana kuwa ndani ya Azam FC.

“Vilevile namshukuru Mungu kwa kuniongezea mwaka mmoja kwenye umri wangu, naomba utukufu na mambo mema yaendelee kunitokea ninayofuraha kujiunga na timu ya Azam,” alisema.

Mara baada ya kutimiza umri wa miaka 18, ni rasmi sasa winga huyo wa kushoto ataruhusiwa kuichezea Azam FC kwenye mechi zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kuanzia ile ya Mbeya City, itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi.