KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumatano itakuwa na shughuli pevu kusaka nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi pale itakapochuana na Jamhuri kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15 usiku.

Azam FC ilianza vema michuano hiyo jana kwa kuichapa Zimamoto, bao likifungwa na Shaaban Idd dakika ya 79 akiunganisha krosi safi iliyochongwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mchezo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na aina ya matokeo yanayosakwa na timu zote mbili, Azam FC ikisaka pointi tatu za kuisaidia kutinga hatua ya nusu fainali.

Jamhuri ambayo iliambulia kipigo kizito cha mabao 6-0 jana dhidi ya Yanga, nayo itakuwa ikisaka ushindi ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele kitu ambacho ni kigumu kwa upande wao kutokana na ubora wa kikosi cha Azam FC.

Kauli ya Kocha, Nahodha

Tayari Kocha Mkuu wa muda wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, ameweka wazi kuwa wanauchukulia kwa uzito mchezo huo huku akidai kuwa amerekebisha udhaifu ulijitokeza kwenye mchezo wa awali.

“Wachezaji wangu waliidharau timu pinzani kwenye mchezo wa awali, pia safu ya ushambuliaji ilicheza kwa kuridhika, tayari mechi ya kwanza imewapa somo kwa hiyo nafikiri mechi inayofuatia watafanya vizuri zaidi na kupata matokeo bora,” alisema.

Naye mmoja wa manahodha wasaidizi wa Azam FC, Shomari Kapombe, alisema kuwa wanaenda kupambana kwenye mchezo huo ili kuhakikisha wanaibuka na pointi zote tatu.

“Tunaenda kucheza na Jamhuri, ambayo tumewahi kucheza nayo mara nyingi katika mashindano haya, huwaga mechi zetu na wao zinakuwaga tofauti na watu wanavyotarajia, kwa hiyo sisi tunaendelea na maandalizi na tutaenda kupambana katika mchezo na kupata pointi tatu,” alisema.

Kapombe alitoa wito kwa mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuisapoti Azam FC popote pale walipo na kuiombea kwa Mwenyezi Mungu, ili kesho iweze kufanya kweli kwa kuibuka na ushindi na hatimaye kusonga mbele kwa hatua inayofuata (nusu fainali).

Azam FC itaingia kwenye mchezo ikiwa na urejeo wa winga wake, Joseph Mahundi, aliyepona majeraha ya enka aliyopata wakati Azam FC ikiichapa Tanzania Prisons bao 1-0 katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Msimamo Kundi B

Hadi hivi sasa kuelekea mechi za pili za Kundi B la michuano hiyo, Yanga ndio ipo kileleni ikiwa na pointi tatu sawa na Azam FC lakini inaizidi kwa mabao ya kufunga (tofauti ya mabao matano).

Tofauti hiyo inatokana na Yanga kushinda mabao 6-0 kwenye mchezo wa awali dhidi ya Jamhuri huku Azam FC ikiibuka na ushindi wa 1-0 walipotangulia kucheza na Zimamoto.

Timu za Zimamoto na Jamhuri zote kutoka Zanzibar zilizopoteza mechi zao za awali, zinafuatia kwenye msimamo huo katika nafasi ya tatu na nne zikiwa hazina pointi hata moja.