KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeanza vema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Zimamoto bao 1-0, mchezo uliofanyika jioni hii kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kuongoza Kundi B ikiwa na pointi tatu, ambapo hivi sasa itasubiria mchezo wa pili wa kundi hilo utakazoihusisha Yanga na Jamhuri ili kujua kama itaendelea kukaa kileleni.

Winga wa kushoto wa Azam FC kutoka Ghana, Enock Atta Agyei, alianza kuichezea mechi ya kwanza ya mashindano timu hiyo tokea aliposajiliwa, hii ni baada ya kushindwa kuitumikia kwenye Ligi Kuu kufuatia kutotimiza umri wa miaka 18, ambapo kwenye ligi ataanza kuonekana baada ya kutimiza umri huo Januari 5 mwaka huu.

Azam FC ilibidi isubiri hadi dakika ya 79 kuweza kuandika bao hilo la ushindi lililofungwa na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyeitumia vema pasi ya juu ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii walianza mchezo huo kwa kasi ya chini kabla ya kubadilika dakika 20 za mwisho za kipindi cha pili, ambapo mshambuliaji Samuel Afful, alikaribia kuiandikia bao la uongozi Azam FC dakika ya 30 baada ya kuwatoka mabeki wa Zimamoto lakini shuti alilopiga lilimbabatiza kipa na kuokolewa na mabeki.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote ziliweza kutoka nguvu sawa ya bila kufungana, katika dakika 10 za mwanzo za kipindi cha pili Azam FC ilifanya mabadiliko ya kumtoa Afful na kuingia Shaaban ambaye alienda kufunga bao la ushindi.

Kabla ya kufunga bao hilo, Shaaban huenda angetangalia kufunga jingine kama angekuwa makini kutumia pasi safi ya Enock Atta Agyei dakika ya 59, lakini aliukosa mpira wakati kiwa kwenye harakati za kuupiga mpira.

Azam FC iliweza kuulinda ushindi huo hadi dakika 90 zinamalizika, ambapo itashuka tena dimbani Keshokutwa Jumatano kucheza dhidi ya Jamhuri mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15 usiku.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk 77, Yahaya Mohammed, Samuel Afful/Shaaban Idd dk 50, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 67