KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kufungua pazia la mwaka mpya wa 2017 kwa kucheza mechi yake ya kwanza leo Jumatatu saa 10.15 jioni kwa kukipiga dhidi ya Zimamoto kwenye mchezo wake wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Wakati ikielekea kufungua pazia hilo, mwaka jana haukuisha vizuri kwa timu hiyo baada ya kupata msiba mzito wa kuondokewa na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Marehemu Said Mohamed Abeid, aliyefariki Novemba 7 kufuatia kuugua ghafla.

Mbali na tukio hilo la huzuni, mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz unakukumbusha baadhi ya mambo makubwa yaliyotikisa ndani timu hiyo mwaka jana kwa mfumo wa namba.

 

17 – Hii inawakilisha siku ya Agosti 17, ambapo Azam FC iliweza kutwaa taji la kwanza msimu huu na la kwanza la Ngao ya Jamii kihistoria kwa kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.

Mabao ya Azam FC ambayo yalikuwa ya kusawazisha yalifungwa na Shomari Kapombe na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ huku yale ya mikwaju ya penalti yakiwekwa kimiani na Bocco, Himid Mao, Kapombe na Michael Bolou.

 

29 – Hii inawakilisha siku ya Novemba 29, ambapo Bodi ya Wakurugenzi wa Azam FC ilimchagua aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Nassor Idrissa ‘Father’, kuwa Mwenyekiti mpya wa mabingwa hao akirithi mikoba ya Marehemu Said Mohamed Abeid.

Mbali na kuziba nafasi hiyo, pia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa timu hiyo, Shani Christoms, naye akachaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na kuhitimisha safu ya uongozi wa Azam FC, ambayo chini yao wapo Ofisa Mtendaji Mkuu Saad Kawemba, Meneja Mkuu Abdul Mohamed na Meneja wa timu, Phillip Alando.

 

17 – Hii inamwakilisha winga Farid Mussa, ambaye hupendelea kuvaa jezi namba17, ambapo Jumatano iliyopita Azam FC ilikamilisha taratibu zake za kujiunga na CD Tenerife ya Hispania ukiwa ni usajili wa mkopo.

Farid aliyeondoka nchini usiku wa siku hiyo kuelekea nchini humo, tayari ameshawasili na jambo linalosubiriwa hivi sasa ni kuanza rasmi majukumu yake ndani ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania (Segunda Division).

Hiyo ni rekodi ya aina yake kwa Azam FC kuweza kutoa kijana anayeenda kucheza kwenye nchi inayotamba kisoka hivi sasa, ikisifika kuwa na ligi bora duniani ya La Liga Santander.

 

5 – Wakati bao ikiwa ni bingwa mtetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashriki na Kati (CECAFA Kagame Cup), namba hiyo ni rekodi ya aina yake ambayo Azam FC imeandika msimu uliopita kwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya ngazi ya klabu barani Afrika kwa mara ya tano mfululizo, ikishiriki Kombe la Shirikisho mwaka huu.

Azam FC ilianza kukata tiketi ya kwanza ya kushiriki michuano ya Afrika mwaka 2012, ilipofanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho mwaka 2013.

Ilifanya maajabu ilipoanza kushiriki michuano hiyo baada ya kufika raundi ya pili na kutolewa na AS FAR Rabat ya Morocco kwa jumla ya mabao 2-1, lakini ilikaribia kutinga hatua ya mwisho ya mtoano (play off) kama nahodha wake Bocco angefunga penalti dakika za mwisho, ambayo ingefanya mpira kumalizika kwa sare ya 2-2 na Azam FC ingesonga mbele kwa bao la ugenini.

Kabla ya kufika raundi hiyo Azam FC ilitangulia kuzitoa, Al Nasir ya Juba, Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1 kabla ya kutinga raundi ya kwanza na kuitupa nje Barrack YC II ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1, ushindi iliyoupata ugenini jijini Monrovia.

Mwaka unaofuata ikashiriki tena Kombe la Shirikisho, lakini ikaishia raundi ya awali kwa kutolewa na Ferroviario de Beira kwa jumla ya mabao 2-1, ikianza kuipiga nyumbani (Azam Complex) kabla ya kufungwa ugenini 2-0.

Azam FC ikaishia tena raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka juzi baada ya kutolewa na moja ya vigogo wa Afrika, El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-0 Azam Complex kabla ya kupigwa 3-0 ugenini.

Mwaka jana Azam FC ikajiandikia rekodi ya kuwa timu pekee Afrika Mashariki na Kati iliyoanzia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na hata kwa wale wa Ligi ya Mabingwa, ambapo iliweza kuishia raundi ya pili baada ua kutolewa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda 2-1 nyumbani na kupoteza 3-0 jijini Tunis.

Katika raundi ya kwanza Azam FC iliwatoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3, matajiri hao wakiandika rekodi ya kushinda nyumbani (4-3) na ugenini (3-0).

 

2 – Moja ya jambo lingine kubwa kwa mwaka ulioisha ni Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipanga Azam FC kuanzia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili mfululizo, ikifanya hivyo tena kwenye michuano ya mwaka jana.

Tayari ratiba ya michuano hiyo imetoka ambayo inaonyesha kuwa, Azam FC itaanza kukata utepe kwenye raundi hiyo kwa kukipiga na bingwa wa mechi ya raundi ya awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

 

28 – Hii inasimama badala ya kipa namba moja wa Azam FC, Aishi Manula, ambaye amefanya makubwa kwa mwaka ulioisha baada ya kufanikiwa kutwaa tuzo mbili za kipa bora kwenye michuano miwili mikubwa nchini.

Manula ambaye pia ni kipa wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alichaguliwa kuwa kipa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita baada ya kufanya vizuri sana na aliitwaa kama hiyo kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) akiiongoza Azam FC kushika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga.

 

6 – Hii inawakilisha rekodi ya Azam FC waliyoiandika Septemba 10 walipoifunga Mbeya City 2-1 kwenye msimu huu wa ligi na kubeba pointi sita zote kwa mara ya kwanza ndani ya Uwanja wa Sokoine, Mbeya jambo ambalo ilishindwa kulifanya misimu kadhaa ya nyuma.

Rekodi hiyo ilinogeshwa na kuzoa pointi tatu za kwanza kwa kuwafunga maafande wa Tanzania Prisons (1-0) kwa mara ya kwanza msimu huu ndani ya uwanja huo, bao pekee likiwekwa kimiani na kiungo wa zamani wa timu hiyo Michael Bolou.

 

81 – Hii ni dakika ya bao ambalo liliipa ushindi wa kwanza wa kihistoria wa Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza dhidi ya Toto African ya huko, bao hilo liliwekwa kimiani na Shaaban Idd kufuatia pasi safi ya Bocco, aliyewatoka mabeki kadhaa wa Toto.

 

22 – Hii ndio inafunga tukio kubwa la kufunga mwaka la Azam FC lililofanyika Novemba 22 mwaka huu la kupokea ugeni mzito wa kutembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Paul Makonda, ndani ya makao makuu ya Azam Complex.

Mbali na Makonda kufurahishwa na mazingira aliyoyakuta Azam FC, pia alimpongeza mfanyabiashara mashuhuri Afrika Mashariki na Kati na Afrika kwa ujumla, Alhaji Said Salim Bakhresa, kwa uwekezaji alioufanya ndani ya timu hiyo na katika Makampuni ya Bakhresa.

Alisema uwekezaji wake umefanikisha kutengeneza ajira nyingi kwa Watanzania, hivyo akatoa rai kwa Watanzania wote kusapoti na kununua bidhaa zinazotengenezwa kwenye viwanda vya hapa nchini na Watanzania wazalendo akimtolea mfano Bakhresa kutokana na juhudi anazofanya.