KOCHA Mkuu wa muda wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia kuwa kikosi chake kipo imara kuanza kazi ya kuwania taji la Kombe la Mapinduzi.

Cheche ametoa kauli hiyo, mara baada ya kikosi hicho kumaliza mazoezi ya mwisho leo asubuhi kwenye Uwanja wa Dimani visiwani Zanzibar kabla ya kesho Jumatatu kufungua dimba kwa kuvaana na Zimamoto kwenye Uwanja wa Amaan saa10.15 jioni.

“Kwanza tumejipanga vizuri na kikosi change chote kipo imara, kasoro wachezaji wawili Mahundi (Joseph) na Mcha (Khamis), ambao wana majeraha madogo, lakini wote waliobakia ni kikosi kinachojitosheleza kabisa kwa ajili ya mashindano kwa kuanzia mchezo wetu wa kesho dhidi ya Zimamoto,” alisema.

Mbali na Azam FC kuwakosa nyota wake hao wawili, pia itaendelea kumkosa beki wake wa kushoto Gardiel Michael, ambaye hivi karibuni ametolewa plasta gumu ‘P.O.P’ kwenye mkono wake na kwa sasa anaendelea na programu ya mazoezi binafsi ya uwanjani mpaka pale atakaporejea katika hali yake ya kawaida.

Cheche alichukua fursa hiyo pia, kuwakaribisha mashabiki wa soka wajitokeze kwa wingi kuwaangalia kwani wamejipanga vilivyo kurejesha heshima ya timu kwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

“Timu zote zimejipanga kushinda na sisi tumejipanga kushinda, kikosi kipo imara na vijana wapo kwenye hali ya utulivu kabisa, mimi nafikiri tusiandikie mate kesho watu wote wajitokeze waje kuona, kwa sababu tumejipanga vilivyo kurudisha heshima yetu na tunaanzia kesho dhidi ya Zimamoto, wapenzi wetu waliokata tamaa kidogo waje kwani timu yetu imerudi vizuri,” alisema.

Azam FC inayoshikilia rekodi ya aina yake kwenye michuano hiyo ikiwa ni timu pekee iliyolitwaa taji hilo mara mbili mfululizo 20012 na 2013, imejiwekea malengo ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo kwa kufika hatua za mbali ikiwemo kutwaa taji hilo.