KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kipo visiwani Zanzibar tokea saa 12 jioni kikiwa kimewasili na morali kubwa ya kutwaa taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Azam FC imefikia katika Hoteli ya kifahari na ya kisasa inayotamba hivi sasa Visiwani Zanzibar ya Mtoni Marine, inayomilikiwa na mmoja wa wafanyabishara maarufu Afrika Mashariki na Kati na Afrika kwa ujumla, Alhaji Said Salim Bakhresa.

Matajiri hao watafungua dimba la michuano hiyo kwa kuvaana na Zimamoto keshokutwa Jumatatu saa 10.15 jioni ndani ya Uwanja wa Amaan Zanzibar, na ipo Kundi B pamoja na timu nyingine za Yanga na Jamhuri.

Kikosi kilichowasili kinaundwa na wachezaji; makipa Aishi Manula, Mwadini Ally na Metacha Mnata, mabeki Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Abdallah Kheri, Ismail Gambo, Gardiel Michael.

Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Stephan Kingue, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, mawinga Joseph Mahundi, Ramadhan Singano ‘Messi’, Enock Atta Agyei na washambuliaji Yahaya Mohammed, Samuel Afful.

Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ na Msaidizi wake, Himid Mao ‘Ninja’, wenyewe wanatarajia kujiunga na kikosi hicho kesho Jumapili.

Mabeki wawili Daniel Amoah, amepewa ruhusa maalumu ya kwenda nchini kwao Ghana huku Bruce Kangwa akijiunga na timu yake ya Taifa ya Zimbabwe ‘The Warriors’ inayojiandaa kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon.

Kwa mujibu wa programu chini ya makocha wa muda wa Azam FC, Idd Nassor Cheche na Idd Abubakar, inaonyesha kuwa kikosi hicho kitafanya mazoezi ya kwanza visiwani humo kesho saa 3.00 asubuhi ndani ya Uwanja wa Amaan kabla ya kukipiga na Zimamoto siku inayofuata.