KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Majimaji kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, Ruvuma.

Azam FC iliyofanikiwa kucheza vema kipindi cha kwanza, ilianza kuliona lango la wapinzani wao kwa kupata bao la uongozi dakika ya 8 tu, lililofungwa kiufundi na straika mpya Yahaya Mohammed, akimalizia pasi safi ya Joseph Mahundi.

Hilo ni bao lake la kwanza kwenye ligi ndani ya mechi mbili alizocheza tokea asajiliwe kwenye dirisha dogo akitokea Aduana Stars ya Ghana, bao jingine alifunga katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar (2-2).

Tatizo la Uwanja wa Majimaji kutokuwa vizuri kwenye eneo la kuchezea, lilizilazimu timu zote mbili kucheza soka la mipira ya juu sana, jambo ambalo lilifanya mpira kutokuwa mzuri kwa dakika zote tisini.

Majimaji ilibadilika sana kipindi cha pili, jambo ambalo liliwapatia bao la kusawazisha dakika ya 66 lililofungwa na Alex Kondo kwa kichwa akimalizia mpira wa kona.

Azam FC ilifanya jitihada kusaka bao la ushindi, ambapo dakika ya 76 Bocco alitumia akili binafsi kuwatoka walinzi wa Majimaji, lakini shuti alilopiga liligonga mwamba kabla ya kuokolewa.

Hadi dakika 90 zinamalizika, timu zote ziliweza kugawana pointi moja na kila upande kuacha pointi mbili uwanjani.

Sare hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 27 na kuteremka kwa nafasi moja hadi ya nne ikizidiwa pointi 14 na kinara Simba (41), huku Kagera Sugar ikipanda hadi ya tatu baada ya kufikisha pointi 28.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, wanatarajia kushuka tena dimbani Alhamisi ijayo Desemba 29 kukipiga dhidi ya maafande wao Tanzania Prisons, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Kikosi kilikuwa hivi:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Himid Mao dk 62, Frank Domayo/Shaaban Idd dk 79, Yahaya Mohammed, John Bocco, Bruce Kangwa/Ramadhan Singano dk 70