WAKATI kikosi cha Azam FC kikiwa safarini hivi sasa kuelekea mkoani Ruvuma kukabiliana na Majimaji, habari njema ni kuwa hadi kufikia leo jioni Jumatano kinatarajia kujua mpinzani atakayepangwa naye kwenye kinyang’anyiro cha kuwania taji la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, ndio iliyokata tiketi ya kushiriki michuano hiyo mwakani baada ya kukamata nafasi ya pili kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kufuatia kupoteza mchezo wa fainali kwa kufungwa na Yanga mabao 3-1.

Yanga ndio waliokuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambao nao watajua mpinzani watakayepangiwa naye kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hafla ya upangaji wa ratiba ya michuano hiyo yote, inatarajia kufanyika jijini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambao ndio waandaaji wakuu wa michuano hiyo.

Tanzania ni moja ya Mataifa 35 ya Afrika, ambayo yananafasi moja tu ya kuingiza timu katika kila michuano hiyo ya klabu, huku mataifa mengine makubwa 12 yaliyo na alama nyingi hupewa nafasi za kuingiza timu mbili katika kila michuano.

CAF kuelekea michuano ya mwakani imebadilisha mfumo wa mashindano hayo, ambapo imepanua wigo kwa timu zitakazoingia hatua ya makundi kutoka nane hadi 16, kila michuano itahusisha makundi manne yenye timu nne kila moja.

Mfumo huo unamaanisha kuwa timu 32 zitakazocheza raundi ya kwanza inayofuata baada ya ile ya awali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, zile 16 bora zitakazoshinda zitaingia moja kwa moja katika hatua ya mwisho ya mtoano (play off).

Katika hatua hiyo zitakutanishwa na timu nyingine 16 zilizotolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na wale 16 bora watakaopenya hapo watafuzu moja kwa moja kwenye hatua ya makundi, itakayoanza kuchezwa Mei mwakani.

Azam FC imekuwa na kiu kubwa ya kufika hatua ya makundi katika michuano hiyo mikubwa ya ngazi ya klabu Afrika itakayokuwa ikishiriki kwa mara ya nne hapo mwakani, mara tatu Kombe la Shirikisho na mara moja Ligi ya Mabingwa.

Azam FC kuanzia raundi ya kwanza?

Mwaka huu, Azam FC iliandika rekodi ya kuwa timu pekee ya Afrika Mashariki kuanzia raundi ya kwanza kwenye michuano hiyo na hata kwa wale walishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, zingine zote za ukanda huo zilianzia raundi ya awali.

Azam FC kwenye raundi ya kwanza ilikutana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini na kuitoa kwa jumla ya mabao 7-3, ikiwafunga ugenini mabao 3-0 na kuwapa kipigo kingine cha nyumbani 4-3.

Raundi ya pili mabingwa hao wakakutana na vigogo wa Tunisia, Esperance na kujikuta ikifa kiume kwa kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2.

Je, mwaka huu Azam FC itapangwa kuanzia raundi gani? Ni jambo la kusubiri, endelea kutembelea mtandao huu wa www.azamfc.tz kuweza kujua hilo.

Rekodi ya Azam Complex balaa

Licha ya Azam FC ambayo bado ni timu changa kwenye michuano hiyo ya Afrika kushindwa kufika hatua ya makundi, tayari imeshajiwekea rekodi kubwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex, ambapo haijawahi kupoteza mchezo wowote wa michuano hiyo.

Mara nyingi imekuwa ikipoteza ugenini kwa baadhi ya michezo, lakini nyumbani ina ushindi wa asilimia 100.

Ilianza kuufungua uwanja huo kwenye mechi za kimataifa kwa kuwatandika Ferroviario de Beira bao 1-0 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho mwaka 2013 lililofungwa na Kipre Tchetche, lakini ikatolewa kwa kufungwa 2-0 ugenini.

Azam FC mwaka juzi ikawakaribisha moja ya vigogo wa Afrika kutoka Sudan, El Merreikh na kuwafunga 2-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mabao ya Didier Kavumbagu na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, lakini haikuwa na bahati baada ya kufungwa mabao 3-0 ugenini.

Mwaka huu ikakutana na vigogo wengine, Esperance kwenye raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho na kuwapa kipondo cha mabao 2-1 nyumbani yaliyofungwa na Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’, kabla ya kupoteza ugenini kwa kufungwa mabao 3-0.

Kwa upande wa zawadi je?

Kwa mwakani, CAF imepandisha zawadi kwa washindi wa Kombe la Shirikisho, wakati bingwa akivuna Dola za Kimarekani Milioni 1.25 (sawa na zaidi ya Bilioni 2.72 za Kitanzania), mshindi wa pili atajizolea Dola za Kimarekani 625,000 (sawa na zaidi ya Sh. Bilioni 1.36).

Timu zitakazoingia nusu fainali kila mmoja itajizolea Dola za Kimarekani 450,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 979.96), zilizoingia robo fainali nazo zitazoa Dola za Kimarekani 350,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 762.19) huku zile zitakazoshika nafasi ya tatu na nne kwenye makundi zikiambulia Dola za Kimarekani 275,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 598.86).

Timu zinazoweza kukutana na Azam FC?

1) Algeria: JS Kabylie au Mouloudia Alger

2) Cameroon: Apejes Academy au Young Sports Academy

3) Congo Brazzaville: CARA au Etoile

4) Congo DR: Renaissance au Sanga Balende

5) Misri: Al Masry au Smouha

6) Ivory Coast: ASEC Mimosas au Sporting Gagnoa

7) Mali: Djoliba au Onze Createurs

8) Morocco: Ittihad Tanger au Moghreb Fes

9) Nigeria: Ifeanyi Ubah au Wikki Tourists

10) Afrika Kusini: Platinum Stars au SuperSport Utd

11) Sudan: Al Ahly Shendy au Al Hilal Al Obeid

12) Tunisia: Club Africain au CS Sfaxien

13) Angola: Recreativo Libolo

14) Botswana: Orapa United

15) Burkina Faso: Sonebel

16) Burundi: Le Messager Ngozi

17) Jamhuri Afrika ya Kati: Anges Fatima

18) Comoro: Volcan

19) Djibouti: Dikhil

20) Guinea ya Ikweta: Racing Micomeseng

21) Ethiopia: Defence Force

22) Gabon: Akanda

23) Gambia: Brikama United

24) Ghana: Bechem United

25) Guinea: Kaloum

26) Kenya: Ulinzi Stars

27) Liberia: Monrovia Breweries

28) Libya: Al Hilal Benghazi

29) Madagascar: Saint-Michel Elgeco Plus

30) Malawi: Be Forward Wanderers

31) Mauritania: Concorde

32) Mauritius: Pamplemousses

33) Mozambique: Songo

34) Niger: Douanes

35) Rwanda: Rayon Sports

36) Senegal: Niarry Tally

37) Seychelles: Saint-Michel United

38) Sierra Leone: Johansen

39) Somalia: Jeenyo United

40) Sudan Kusini: Al Salam Wau

41) Swaziland: Mbabane Swallows

42) Togo: Koroki Tchamba

43) Uganda: Vipers

44) Zambia: ZESCO United

45) Zimbabwe: Ngezi Platinum