KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni ya leo imeshindwa kufungana na African Lyon katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na mabadiliko makubwa baada ya kujumuishwa kikosini kwa wachezaji watano waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili, ambao ni beki Yakubu Mohammed, kiungo mkabaji Stephan Kingue Mpondo, winga Joseph Mahundi na washambuliaji Yahaya Mohammed, Samuel Afful.

Kipindi cha kwanza kasi ya mchezo ilionekana kuwa chini kwa pande zote mbili, lakini kama si uhodari wa kipa wa Africal Lyon, Youthe Rostand, wa kuokoa michomo huenda Azam FC ingemaliza kipindi hicho ikiwa imefunga mabao matatu kupitia kwa nahodha John Bocco, Afful na Yahaya.

Mabingwa hao wa Ngao Jamii, waliweza kucheza vema kipindi cha pili hasa baada ya kuingia viungo wawili Frank Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kutoka Afful dakika 53 na Mahundi dakika ya 60, ambapo Azam FC ilionekana kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Lyon, ambao muda mwingi wa mchezo walikuwa wakicheza kwa kujihami.

Dakika ya 73, Yahaya alikaribia kuiandikia bao la uongozi wa Azam FC kama si shuti kali alilopiga kugonga mwamba na kuokolewa na mabeki, nyota huyo aliipata nafasi hiyo baada ya kutengenezewa pande safi na Bocco.

Mwamuzi wa mchezo huo alilazimika kuongeza dakika 11 za nyongeza kufuatia mchezo huo kusimama kwa takribani dakika saba kupisha kipa wa Lyon, Rostand kutibiwa ambaye alishindwa kuendelea na kukimbizwa hospitali baada ya kupata maumivu ya mbavu akiwa kwenye harakati za kuokoa shuti lililopigwa na Shomari Kapombe.

Hadi mpira unamalizika timu hizo ziliweza kutoka uwanjani zikiwa hazijaweza kufungana, matokeo ambayo yanaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 26 ikibakia nafasi ya tatu na kuzidiwa pointi 12 na Simba inayoongoza kwa pointi 38 huku nafasi ya pili ikishikwa na Yanga (36).

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitapumzika kwa siku ya kesho kabla ya kurejea mazoezini keshokutwa Jumanne kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Majimaji utakaofanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, mkoani Ruvuma.