TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam FC U-20), usiku wa kuamkia leo imetinga fainali ya michuano ya Ligi ya Vijana ya TFF baada ya kuichapa Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalti 4-2 kwenye mchezo wa nusu fainali, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 na 30 za nyongeza.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC U-20, kukata tiketi ya kuchuana na Simba kwenye mchezo wa fainali kesho Jumapili, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.

Kama ilivyokuwa kwa Azam FC U-20, Simba nayo ililazimika kusubiri hadi changamoto ya kupigiana mikwaju ya penalti ili kuitoa Stand United, kufuatia muda wa kawaida wa mchezo na dakika 30 za nyongeza kuisha kwa sare ya bao 1-1 na hivyo wekundu hao kushinda 8-7.

Washmabuliaji wa Azam FC U-20, Shaaban Idd na Sadalah Mohamed, itabidi wajilaumu wenyewe baada ya kushindwa kumaliza mchezo huo mapema kutokana na kukosa umakini kila walipolikaribia lango la wapinzani wao na kujikuta wakipoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao.

Mchezo huo kwa kiasi kikubwa ulikuwa na ushindani mkubwa kwa pande zote mbili, ambazo zilikuwa zikicheza kwa kasi kila zikipata mpira hali ambayo iliwafanya mabeki wa timu hizo kufanya kazi kubwa ya kuokoa hatari zote.

Safu ya ulinzi ya Azam FC U-20, iliyokuwa chini ya kipa anayeibukia kwa kasi Metacha Mnata, mabeki Abbas Kapombe, aliyekuwa nahodha wa mchezo huo, Joshua Thawe, Godfrey Elias na Ramadhan Mohamed, ilifanya kazi nzuri usiku huo wakihakikisha wachezaji wa Mtibwa hawaleti madhara langoni mwao.

Wachezaji wa Azam FC U-20 walipata penalti zote nne walizopiga kupitia kwa Rajab Odasi, Joshua, Adolf Bitegeko na Shaaban, aliyefunga penalti ya ushindi huku Mtibwa itakayocheza na Stand United kuwania nafasi ya tatu kesho saa 10.00 jioni ikipata mbili tu na kukosa idadi kama hiyo hiyo.

Vijana hao wa Azam FC, waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na mapengo kadhaa ya kuwakosa wachezaji wake tegemeo katika eneo la kiungo, nahodha Abdallah Masoud ‘Cabaye’, Prosper Joseph, mabeki Mohamed Omary, Said Issa, waliokuwa na kadi mbili za njano na kufanya benchini iwe na upungufu wa wachezaji wanne na kuwa na wachezaji watatu wa kubadilisha akiwemo kipa.

Kikosi cha Azam FC U-20 jana:  

Metacha Mnata, Salum Isihaka/Omary Wayne, Ramadhan Mohamed, Abbas Kapombe, Joshua Thawe, Adolf Bitegeko, Godfrey Elias, Stanslaus Ladislaus/Charles Ndahaze dk 75, Shaaban Idd, Sadalah Mohamed, Rajab Odasi