KOCHA Mkuu wa timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam FC U-20), Idd Cheche, amesema kuwa wataanza na moto mkali zaidi kwenye mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Vijana ya TFF dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam leo Ijumaa saa 1.00 usiku.

Cheche amedai kuwa moto watakaouendeleza ni zaidi ya ule waliouwasha mjini Bukoba, mkoani Kagera uliowafanya kuongoza Kundi B kwa kujikusanyia jumla ya pointi 17 na kutinga nusu fainali kwa kishindo baada ya kushinda mechi tano, sare mbili na kutopoteza mchezo wowote.

“Kikosi tumekipanga vizuri kuelekea mchezo huo kama tulivyotoka kucheza mechi za Bukoba, kadiri tulivyokuwa tukicheza mechi tulizidi kuimarika tofauti na tulivyoanza, namna tulivyomaliza ni tofauti sana na tulivyoanza na kwa sasa hivi tunavyomalizia tutaendelea na moto mkali zaidi ya ule tuliouwasha Bukoba,” alisema Cheche wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Tumeiona Mtibwa Sugar

Akizungumzia namna atakavyoikabili Mtibwa Sugar, iliyomaliza nafasi ya pili kwenye Kundi A ikiwa na pointi 14, kocha huyo alisema kuwa anajua namna ya kukabiliana nao baada ya kuwaona kupitia kingamuzi cha Azam TV, katika mechi zao kadhaa za makundi walizocheza.

“Mimi nafikiri Mtibwa Sugar tumeshawaona, hivyo tutajipanga kujibu mapigo yao kama tulivyojipanga kwenye mechi nyingine tulizocheza kwenye kituo cha Bukoba, naamini kituo chetu cha Bukoba ndio kilikuwa kigumu kuliko cha Dar es Salaam, japokuwa hatusemi kuwa Mtibwa Sugar ni wabaya sana, ni wazuri, tunakubali na kuwaheshimu,” alisema.

Mchezaji huyo aliyetamba zamani na timu za Sigara, Pan African, RTC Kigoma, aliendelea kusema kuwa malengo makubwa waliyojiwekea ni kushinda mchezo huo na kutinga fainali ya michuano hiyo na hatimaye kutimiza lengo kuu la kutwaa ubingwa Jumapili ijayo, itakapopigwa mechi ya fainali saa 1.00 usiku ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

“Matarajio yetu ni kubakisha kikombe hapa, kwa kweli kila kitu huwa kinakuwa kimepangwa, lakini jitihada, uamuzi na ule umoja wetu nafikiri tutafanikiwa japo haitakuwa kazi rahisi, kiukweli tutapambana kufanikisha hilo,” alimalizia.

Azam FC U-20 inayonolewa pia na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, itaingia kwenye mchezo huo ikijivunia wachezaji wake hatari akiwemo mshambuliaji anayeongoza katika chati ya mabao ndani ya michuano hiyo, Shaaban Idd, aliyefunga mabao saba mpaka sasa ndani ya mechi zote saba za makundi alizocheza.

Safu yake ya ulinzi itakuwa imeimarishwa na ulinzi mkali kutoka kwa mabeki wake visiki Abbas Kapombe, Joshua Thawe, Ramadhan Mohamed, Said Issa, na viungo wabunifu Rajab Odasi, Adolf Bitegeko, Omary Wayne, huku Salim Isihaka na Sadalah Mohamed wakisaidiana na Shaaban kwenye eneo la ushambuliaji.

Nusu fainali ya kwanza itakayotangulia saa 10.00 jioni, itashuhudiwa vinara wa Kundi A, Simba wakivaana na Stand United, ambayo ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi B wakiwa na pointi 14 kama ilivyo kwa Mtibwa Sugar Kundi A.