KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa amefurahishwa na viwango vya baadhi ya nyota waliokuja kufanya majaribio ya kujiunga na timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa leo.

Azam FC jana usiku ilimaliza programu ya kukifanyia tathimini kikosi chake kwa kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-1 kwenye mchezo wa kujipima ubavu, ambao pia iliutumia kuwapima wachezaji tisa waliokuja kwa majaribio, mabeki wa kati Nkot Mandeng Eric (Coton Sport De Garoua, Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Asec Mimosa, Ivory Coast).

Kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Coton Sport Garoua, Cameroon), Abdallah Khamis pamoja na washambuliaji Yaya Anaba Joel (Coton Sport Garoua, Cameroon), Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Bernard Ofori (Medeama, Ghana), Konan Oussou (Tala’ea El-Gaish SC, Misri) na Jean Karekezi.

Mabao mawili kati ya matatu ya Azam FC usiku wa jana yalifungwa na nyota waliokuwa majaribio, ambao ni Ofori aliyefunga la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi safi ya Gadiel Michael na Afful akitumia juhudi binafsi kwa kumzidi maarifa beki pemmbeni ya uwanja na kupiga shuti kali lililojaa wavuni.

Hernandez ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa muda kuanzia sasa anatarajia kupeleka mapendekezo yake kwa uongozi wa timu hiyo juu ni nyota gani kati ya hao wasajiliwe, huku akidai kwa viwango alivyoviona anaamini ya kuwa wachezaji watakaosajiliwa wataweza kuisaidia sana Azam FC.

“Raundi ya kwanza imemalizika na tumeona mapungufu ambayo tunataka kuyarekebisha kwa ajili ya raundi ya pili na ndio maana tumejaribu kutafuta wachezaji ambao tunahisi wanaweza kutusaidia kwenye timu raundi ya pili na michuano mingine, kilichobakia sasa hivi tunaamini ya kwamba baadhi ya wachezaji ambao wameonekana wanafaa kabisa kusaidia kwenye timu yetu,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Stanta Ursula ya Hispania, alisema anaamini ya kuwa kikosi chake kikiingia raundi ya pili kitaweza kupambana ipasavyo basi matokeo yatakuwa mazuri na hatimaye kuweza kufikia nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo kuliko nafasi ya tatu ambayo timu hiyo inashika hivi sasa ikiwa na pointi 25 pungufu ya pointi 10 na kinara Simba aliyejikusanyia 35 huku Yanga akiwa nazo 33 (nafasi ya pili).

“Hapa hatukuja kwa ajili ya starehe tumekuja kikazi, tunaamini nafasi ambayo tunayo tunapointi nyingi ambazo tunatakiwa kuzikamilisha ili kuweza kuwafikia hao ambao wapo juu Simba na Yanga, tumejua makosa yetu tuliyofanya raundi ya kwanza na ndio haya tunayafanyia kazi hivi sasa ili kuweza kuyakamilisha, ili hatimaye tuweze kufanya vizuri na hatimaye kuchukua ubingwa, kwa hiyo ni muda ambao tunajiandaa kwa kuziba mapengo ambayo yapo na kuweza kuingia kwenye ushindani zaidi,” alimalizia.

Mara baada ya mchezo wa jana dhidi ya Ruvu Shooting, benchi la ufundi la Azam FC limewapa mapumziko ya wiki mbili wachezaji wa kikosi hicho kabla ya kuanza tena mazoezi Desemba 3 mwaka huu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa.