KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yeray Romero, amesema kuwa ushindi wa mabao 4-1 walioupata dhidi ya Mwadui jana ni muhimu kwa kikosi hicho, akidai ni zawadi tosha ya kumuenzi aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo, Mzee Said Mohamed Abeid, aliyefariki dunia Jumatatu iliyopita jioni.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Shaaban Idd aliyefunga mawili na Francisco Zekumbawira, huku lile la Mwadui likiwekwa nyavuni na Hassan Kabunda.

Romero ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wameondokewa na mtu muhimu kwenye klabu, hivyo ushindi huo unawafanya kujumuika naye pamoja katika kumuenzi.

“Ushindi tulioupata ni mkubwa, kilichotokea ni wachezaji wamejaribu kuona yale madhaifu yaliyotokea na wameyafanyia kazi kwani tuliweza kutanguliwa kufungwa bao lakini wachezaji wakaja juu na kupambana na mabadiliko tuliyofanya kipindi cha pili yaliweza kutupa ushindi huo mnono.

“Kiufupi kipindi cha kwanza kulikuwa na mapungufu yaliyoonekana, kipindi cha pili sisi walimu tulikitumia kurekebisha tuliweza kumuingiza Shaaban (Idd) na Francisco (Zekumbawira) lakini pia Singano (Ramadhan) alitangulia kuingia, tatizo lililoonekana kipindi cha kwanza ni umaliziaji lakini mabadiliko hayo yaliweza kuufanya mchezo kuwa rahisi kwetu na kupata mabao hayo,” alisema.

Ushindi huo umewafanya mabingwa hao kutimiza jumla ya 25 na kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.