MAMIA ya wadau wa soka jioni ya leo wameshiriki mazishi za aliyekuwa Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Mohamed Abeid, aliyefariki jana jioni kwenye Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.

Sheikh Said aliyekuwa pia Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, alizikwa katika makaburi ya Kisutu, jirani na msikiti wa Maamour, Upanga ambako mwili wake ulisaliwa baada ya sala ya Alasiri.

Mwenyekiti wa Makampuni ya Bakhresa Group, wamiliki wa Azam FC, Alhaj Sheikh Said Salim Bakhresa, alihudhuria mazishi hayo pamoja na wanawe wakiwemo, Mkurugenzi Mkuu wa makampuni hayo, Abubakar na Yusuf Bakhresa.

Sura za viongozi wa klabu na vyama mbalimbali vya michezo nchini, wanachama maarufu wa klabu za soka na wafanyakazi wa makampuni mbalimbali ya Bakhresa Group wakiwemo wachezaji wa timu za vijana na Azam ndizo zilizotawala wakati wa mazishi hayo.

Wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Azam FC hawakuwepo kwa sababu wapo na timu hiyo Mwadui, Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na wenyeji, Mwadui kesho.

Sheikh Said Mohamed Abeid atakumbukwa kwa makubwa aliyofanya ndani ya makampuni ya Bakhresa ikiwemo klabu ya Azam FC, aliyoiongoza kuchukua mataji tofauti makubwa kipindi cha uongozi wake tokea timu hiyo ipande daraja mwaka 2008.

Baadhi ya makombe hayo makubwa ni ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14 walioutwaa kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa mchezo hata mmoja, pia mataji mawili ya Kombe la Mapinduzi, ubingwa wa KLabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) mwaka jana na taji la Ngao ya Jamii mwaka huu.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Sheikh Said Mohamed Abeid mahali pema peponi, Amin.

 

N.B: Stori, Picha kwa msaada wa Binzubery Blog