WACHEZAJI wa Azam FC wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwenyekiti wa timu hiyo, Said Mohamed Abeid, kilichotokea jana kwenye Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam.

Nyota hao tokea jana walipopata taarifa ya kifo chake hadi hivi sasa wapo kwenye majonzi makubwa, wakimuelezea Mzee Said kuwa alikuwa ni Baba yao mlezi kutokana na msaada mkubwa aliokuwa akiutoa ndani ya timu hiyo.

Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amesema kwa kumuenzi wanamtakia safari njema Baba yao huyo huko aendako kwenye maisha yake mapya huku akidai wao kama wachezaji wamejipanga kupambana kwenye mchezo wa kesho Jumatano dhidi ya Mwadui ili kupata ushindi na kumuenzi vema Mzee Said Mohamed.

Kikosi hicho kinatarajia kufanya mazoezi ya mwisho leo saa 10.00 jioni ndani ya Uwanja wa Mwadui mkoani hapa kabla ya kupambana na wenyeji wao hao kesho saa 10.30 jioni ukiwa ni mchezo wa kiporo.

Mzee Said Mohamed anayetarajia kuzikwa leo saa 10 jioni kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, atakumbukwa kwa mengi aliyoifanyia timu hiyo ikiwemo kushiriki kwa kiasi kikubwa kwenye mafanikio ya kutwaa makombe muhimu kwenye historia ya Azam FC tokea ilipoanzishwa miaka tisa iliyopita hadi inapanda daraja mwaka 2008.

Baadhi ya makombe hayo makubwa ni ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14 walioutwaa kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa mchezo hata mmoja, pia mataji mawili ya Kombe la Mapinduzi, ubingwa wa KLabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) mwaka jana na taji la Ngao ya Jamii mwaka huu.