KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ametaja sababu ya kikosi chake kupoteza mchezo wa jana dhidi ya Mbao, akidai kuwa kikosi chake kutocheza vema na maamuzi mabovu ya waamuzi vimepelekea kipigo hicho.

Azam FC ilishuhudiwa ikitoka uwanjani bila kuibuka na pointi tatu baada ya kufungwa na Mbao mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba.

Hernandez ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kikosi chake kilijiamini sana katika mchezo huo kuliko wapinzani wao na kujikuta kikishindwa kucheza katika kiwango kilichotarajiwa.

“Kiwango tulichocheza ni tofauti sana na tulichotarajia kukioonyesha, wachezaji walijiamini sana kuliko wapinzani, lakini tatizo jingine kubwa lililoonekana ni ubovu wa waamuzi waliochezesha, walikuwa wanaamua wao tu namna ya kuchezesha mchezo huo,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alizungumzia mfumo alioutumia wa 3-5-2 kama ulikiathiri kikosi chake, ambapo amedai kuwa tatizo halikuwa mfumo bali ni masuala tu ya mchezo na waamuzi kushindwa kufanya kazi yao ipasavyo.

“Mfumo haukupelekea hata kidogo kubadilisha mchezo na kufungwa, ukiangalia mabeki tuliowatumia mechi zilizopita asilimia kubwa ni wale wale, mfumo ukiwekwa haimaanishi itakuwa ngumu kumiliki mpira na kupata ushindi cha msingi.

“Mfumo unaweza kuwepo na mchezaji mmoja mmoja wakitimiza majukumu yao uwanjani ndio inayotakiwa kubadilisha mchezo, kikubwa ninachoweza kurudia sisi hatukuwa na ari ile kama tuliyokuwa nayo mwanzo ya kucheza mpira siwezi kujua nini kimetokea lakini pia aneo la waamuzi nalo limechangia kupatikana kwa matokeo hayo,” alimalizia.

Moja ya udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na waamuzi wa mchezo huo wakiongozwa na mwamuzi wa kati Jacob Adongo kutoka mkoani Mara ni kuruhusu bao la kwanza la Mbao ambalo ni kuotea ‘offside’ lililofungwa na Venance Ludovick dakika ya 29.

Matokeo hayo yameifanya Azam FC kubakiwa na pointi zake 22 na kushuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo kufuatia ushindi wa mabao 3-1 walioupata wa Kagera Sugar jana dhidi ya Ruvu Shooting huku ikizidiwa pointi 13 na vinara wa ligi Simba waliojikusanyia jumla ya pointi 35.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza rasmi safari ya kuelekea mkoani Shinyanga saa 2 asubuhi, kwa ajili ya kucheza mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Mwadui, ambao ni wa kiporo uliopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Mwadui Novemba 9 mwaka huu.