KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imeteleza ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Mbao.

Azam FC ilijikuta ikiruhusu bao ndani ya dakika 30 za mwanzo za kipindi cha kwanza lililofungwa na Venance Ludovick dakika ya 29.

Baada ya kuingia bao hilo, Azam FC ilijitahidi kuzidisha presha ndani ya lango la wapinzani wao, lakini safu ya ulinzi ya Mbao iliweza kuondoa hatari zote.

Kama kiungo Mudathir Yahya angekuwa makini dakika ya 39 huenda angeisawazishia bao timu hiyo baada ya kupata nafasi nzuri akiwa ndani ya boksi kufuatia kupenyezewa pasi nzuri na Gonazo Ya Thomas, lakini shuti alilopiga lilitoka sentimita chache ya lango la Mbao.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Mbao iliweza kuwa mbele kwa bao hilo, Azam FC ilirejea kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili, wakitoka Gadiel Michael, Thomas na kuingia Bruce Kangwa na Ramadhan Singano.

Mabadiliko hayo yaliweza kuongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC, lakini wakati timu ikiwa katika mipango ya kusawazisha bao hilo ilijikuta ikifungwa bao la pili lilifungwa na Boniphace Maganga, dakika ya 50 aliyetumia uzembe uliotokea kwenye eneo la ulinzi la mabingwa hao.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alifanya mabadiliko mengine ya haraka ya kuiongezea uhai safu yake ya ushambuliaji kwa kumuingiza Francisco Zekumbawira na kumtoa Salum Abubakar dakika ya 56, mabadiliko yaliyoiongezea uhai safu hiyo.

Zekumbawira aliweza kuifungia Azam FC bao pekee dakika ya 67 akipiga shuti la kiufundi akimalizia pasi safi ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Mwamuzi wa mchezo wa leo, Jacob Adongo kutoka mkoani Mara, alionekana kushindwa kufuata sharia 17 za soka baada ya kushindwa kuwaonya wachezaji wa Mbao waliokuwa wakipoteza muda kwa makusudi.

Mbali na matukio ya kupoteza muda, pia dakika 89 aliinyima penalti Azam FC baada ya mchezaji wa Mbao, Yousouf Ndikumana, kumtegeshea mguu Mudathir aliyekuwa akipiga shuti kufunga bao, hali iliyofanya wote wawili kuumia.

Pia kuelekea mwishoni mwa mchezo huo, Mwamuzi wa Akiba Mathew Akrama kutoka Mwanza, alimpa maelekezo mwamuzi wa kati Adongo amtoe benchini Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, ambaye alifuata maagizo yake.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kubakiwa na pointi zake 22 na kushuka kwa nafasi moja hadi ya nne kwenye msimamo ikizidiwa pointi 13 na kinara Simba mwenye pointi 35.

Kikosi cha Azam FC kitaanza safari ya kuelekea mkoani Shinyanga kesho asubuhi kwa ajili ya kwenda kukipiga na Mwadui, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mwadui Novemba 9.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, David Mwantika, Frank Domayo, Salum Abubakar/Zekumbawira dk 56, Gadiel Michael/Bruce Kangwa dk 46, Himid Mao, Mudathir Yahya, John Bocco (C), Gonazo Ya Thomas/Singano dk 46