NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amewashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kuendelea kuwaunga mkono huku akiwaahidi kufanya vizuri katika mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Mbao.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa Mwanza ni muhimu kwa Azam FC katika kujiweka pazuri zaidi kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Bocco ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mbali na kunuia ushindi katika mchezo huo, pia amedai moja ya malengo yao ni kufanya vizuri katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Mwadui utakaofanyika Novemba 9, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

“Kwanza tunashukuru kwa sapoti yao, tumepitia kipindi kigumu sana cha nyuma kabla ya mechi tatu zilizopita, walizidi kutusapoti na hawakuweza kutukatisha tamaa, tunashukuru kwa hilo na tunaomba wazidi kutusapoti na kutuamini kuwa tunaweza kufanya vizuri kwa mchezo wa kesho (Mbao) na mchezo unaokuja (Mwadui),” alisema.

Nahodha huyo wa kihistoria wa timu hiyo, alisema kuwa wanawaheshimu wapinzani wao Mbao na kila timu watakayocheza nayo kwenye ligi huku akidai kuwa dakika 90 zitaamua mchezo huo.

“Maandalizi yetu kwa ujumla ni mazuri, tumefanya mazoezi mazuri morali yetu wachezaji ipo vizuri, tunaamini kilichobaki tunasubiri siku ya kesho ifike tuweze kwenda kupigana kwa ajili ya pointi tatu…Kila timu iliyopo Ligi Kuu ni timu nzuri, ligi ni ngumu kila timu imejiandaa vizuri, sisi tunachokiangalia ni maandalizi yetu,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachochangamsha mwili na kuburudisha koo pamoja na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa ya kushinda mechi tatu zilizopita zikiwemo mbili za Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar (3-2) na Toto African (1-0).