TIMU ya Vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam U-20’ inatarajia kufungua dimba na vijana wenzao wa Mbao FC Novemba 17 mwaka saa 8.00 mchana, katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Vijana ya Taifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Ligi hiyo itakayoanza Novemba 15, inaandaliwa na TFF kwa ushirikiano na Kampuni ya Azam Media Limited inayotoa vingamuzi bora vya Azam TV, ambayo imemwaga Sh. Bilioni 2 kwa ajili ya kuonyesha moja kwa moja ligi hiyo pamoja na ile ya wanawake iliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Azam U-20 imepangwa Kundi A kwenye kituo cha mjini Bukoba, mkoani Kagera pamoja na timu nyingine za Mbao, Yanga, Kagera Sugar, Stand United, Mwadui, Toto Africans na African Lyon.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu Idd Cheche, kilikuwa kwenye maandalizi makali kuelekea ligi hiyo na moja ya mipango ya mtaalamu huyo, ni kuhakikisha wanaondoka na ubingwa kama walivyofanya katika michuano mingine ya vijana ya Uhai Cup miaka michache iliyopita.

Mbali na kundi hilo, Kundi B litakalokuwa kwenye kituo cha Dar es Salaam, limeundwa na timu za Simba, Ndanda, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Tanzania Prisons, Mbeya City, Majimaji na Mtibwa Sugar.

Ligi hiyo ya mkondo mmoja inatarajiwa kuhitimisha hatua ya makundi Desemba 12 mwaka huu, ambapo timu nne vinara katika kila kundi zitapangiwa ratiba mpya na kituo ili kutafuta bingwa wa msimu wa kwanza kwa timu za vijana.

Ujio wa ligi hiyo ni utekelezaji au kukidhi matakwa ya maelekezo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), katika kipengele cha uwepo wa timu za vijana zinazoshindana mbali ya kupata huduma za shule na matibabu kwa timu zote za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).