KIWANGO kizuri anachoendelea kufanya mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Idd, kimetosha kabisa kumfanya kumuaminisha Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Zeben Hernandez, kumtabiria makubwa kinda huyo akidai atakuwa staa wa baadaye wa timu hiyo.      

Idd aliendeleza makubwa kwenye mchezo wa jana dhidi ya Toto African baada ya kufunga bao pekee liliwapa ushindi Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati Toto African (1-0).

Itakumbukwa kuwa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, kinda huyo pia alitoa krosi safi iliyozaa bao la ushindi la Azam FC dhidi ya Kagera Sugar (3-2), lililowekwa kimiani kwa kichwa safi na nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Hernandez alisema kuwa kinda huyo anatakiwa kuendelea kusaidiwa ili aweze kuboreshwa na kutumika vizuri zaidi baadaye, huku akidai kazi hiyo ndio wanayoifanya hivi sasa ya kumfikisha kwenye uwezo wa juu.

“Benchi la ufundi tumeliona hilo na tunaendelea kumsaidia kwa kila ambavyo inawezekana ili kuweza kubakisha hadhi yake na kupata kiwango bora zaidi tofauti na hapa ambapo yupo.

“Shaaban ni staa wa baadaye wa Azam FC, kwanza anaweza kuuchezea mpira, tumejaribu kumpa nafasi baada ya kumtoa kwenye kikosi chetu cha vijana, kiukweli ni kwamba anavyocheza anasaidia kwa sababu si leo tu (jana) anafunga bao, hata mchezo uliopita alipiga krosi iliyotupa bao la ushindi,” alisema.

Kinda huyo ni zao la kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam Academy’, kilichotoa nyota wengine wanaotamba na timu kubwa ya kikosi hicho kama vile mabeki Gadiel Michael, Ismail Gambo, viungo Mudathir Yahya, Abdallah Masoud, na winga Farid Mussa, ambaye muda wowote atajiunga na Club Deportivo Tenerife ya Hispania kuanza maisha mapya ya soka barani Ulaya.                       

Anavyouzungumzia mchezo vs Toto

Mbali na ushindi huo kuifanya Azam FC kuandika rekodi ya kushinda kwa mara ya kwanza dhidi ya Toto African kwenye ligi ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba tokea ipande daraja mwaka 2008, Hernandez amedai kuwa walikutana na ugumu wa aina yake kutokana na ubovu wa uwanja huo kutoruhusu kuonyesha soka lao walilozoea.

“Uwanja umetupa ugumu kucheza kwani ni tofauti na ule tuliouzoea, lakini jambo jingine tumekutana na changamoto ya baadhi ya majeruhi ambao ni muhimu sana kwenye timu, mfano Kapombe (Shomari), Bruce (Kangwa), Aggrey (Morris), na Himid (Mao) mwenye adhabu ya kadi nyekundu.

“Kikubwa tunashukuru tumeondoka na pointi zote tatu kwa sababu wachezaji wamejitahidi kwa uwezo wao na wamejaribu kuwa na nidhamu nzuri mchezoni na walipambana kwa muda wote na mwisho tukaondoka na ushindi huo,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, aliongeza kuwa cha muhimu si wao kuvunja rekodi bali ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi, lakini hakuacha kuwapongeza wachezaji wake kwa kufanikiwa kuvunja mwiko huo kwa kuibuka kidedea.

“Kuvunja rekodi kwetu ni jambo la kawaida na wala hatuangalii sana hilo, tunachoangalia hivi sasa sisi ni kupata pointi tatu ili kuzidisha pointi na kufika kwenye nafasi zile ambazo tunazitegemea, tunafurahi kwa rekodi ambayo imevunjwa na kikubwa zaidi ni kwamba tunawashukuru sana wachezaji kwa sababu wao ndio wameonyesha jitihada kwa kupambana na kuvunja rekodi,” alisema.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC leo hii kimeendelea na mazoezi mepesi ya kurudisha mwili kwenye hali yake ya kawaida baada ya kazi kubwa waliyoifanya jana, ambapo Jumapili ijayo inatarajia kushuka tena dimbani kuvaana na Mbao ndani ya dimba hilo la hapa jijini Mwanza.